Nyenze ataka Duale afunguliwe mashtaka ICC

Wabunge wa Ukambani

Marehemu Francis Nyenze (pili kutoka kushoto) na wabunge wengine wakihutubia wanahabari awali. Picha/DIANA NGILA 

Na THOMAS WAITA

Imepakiwa - Sunday, January 8  2017 at  14:28

Kwa Mukhtasari

MBUNGE wa Kitui Magharibi Francis Nyenze ameitaka Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kumfungulia mashtaka Mbunge wa Garissa Mjini Aden Duale kwa kile alichotaja kama majaribio ya kuanzisha mauaji ya halaiki.

 

Akizungumza na wanahabari mjini Kitui Ijumaa, Bw Nyenze (pichani) alishutumu kiongozi huyo wa walio wengi Bungeni kwa kuchochea Wasomali dhidi ya Wakamba wanaoishi Garissa.

Hii ni baada ya sauti iliyodhaniwa kuwa ya Duale kusambazwa katika mitandao ya kijamii Alhamisi.

“Ninaiomba ICC kumchunguza na kumfungulia mashtaka Aden Duale kwa uchochezi wa kijamii dhidi ya Wakamba hasa wakati huu ambapo taifa hili linangojea Uchaguzi Mkuu wa Agosti 8,” alisema.

Mshukiwa katika sauti hiyo ambayo haina siku anaaminika kuwa Bw Duale. Anasikika akiwashauri vijana Garissa kuwazuia Wakamba kujisajili kama wapigakura na kueneza siasa za Chama cha Wiper katika Eneo Bunge la Garissa Mjini.

Sauti hiyo ilisambazwa kwa wingi Alhamisi huku watumiaji wa mitandao ya kijamii wakitoa wito wa kukamatwa kwa Bw Duale kwa madai ya uchochezi.

Bw Duale hata hivyo alikana madai hayo na kusema ilikuwa propaganda kutoka kwa washindani wake wa kisiasa.