http://www.swahilihub.com/image/view/-/3499332/medRes/1521959/-/i5s1yn/-/moka.jpg

 

Seneta Mong'are mbioni kuandaa mswada wa kumtimua rais

Kennedy Mong'are

Seneta wa Nyamira Kennedy Mong'are Okong'o ahutubia wanahabari katika hoteli ya Serena, Nairobi baada ya kutangaza kuingia ulingoni kuwania urais Desemba 27, 2016 

Na WANDERI KAMAU

Imepakiwa - Sunday, January 8  2017 at  20:26

Kwa Mukhtasari

SENETA wa Nyamira Kennedy Mong’are amesema kuwa amekamilisha rasmi uandaaji wa mswada wa kumwondoa mamlakani Rais Uhuru Kenyatta.

 

Aidha, alisema kuwa amezungumza na wabunge 10, ambao wako tayari kuwasilisha mswada huo Bungeni ili kujadiliwa. “Wabunge hao wamejitolea kuniunga mkono bila kujali miegemeo yao ya kisiasa.

Lengo langu kuu ni kuwakomboa Wakenya kutokana na mzongo wa changamoto zinazowakabili,” akasema jana, kwenye kikao na wanahabari jijini Nairobi.

Alieleza kuwa atatumia njia huru kuwashinikiza wabunge kumuunga mkono, kwani mswada huo unalenga kuirejesha nchi katika “hali yake ya kawaida.”

Alitaja mgomo wa madaktari, hali ya njaa katika baadhi ya sehemu nchini, hali ya ufisadi Serikalini, ukabila kati ya masuala mengine kama baadhi ya majukumu ambao rais amekosa kuyawajibikia.

Alisema kuwa rais anaonekana kutojali, huku mamia ya Wakenya wakiendelea kufariki kutokana na mgomo wa madaktari.

“Ni dhahiri kwamba kutotatuliwa kwa mgomo huo kunawanyima Wakenya haki ya kuishi, kulingana na Kipengele 26 cha Katiba, ambacho kinaihitaji Serikali kutoa huduma muhimu kama afya kwa kila Mkenya. Hii ni sawa na kuwaua, kinyume na kuyalinda maisha yao,” akasema Bw Mong’are.

Alieleza kuwa kwa ujumla, Rais Kenyatta amekiuka vipengele 16 vya katiba, hilo likiwa kinyume na kiapo chake cha kuilinda na kuitetea.

Aliilaumu Serikali ya Jubilee kwa kukosa kushughulikia matatizo yaliyoikumba Kenya tangu uhuru, na badala yake ikiyaongeza kupitia ukabila, viwango vya juu vya ufisadi na ukosefu wa ajira.

Wakenya wazinduke

“Wakati umnetimia Wakenya wazinduke ili kuikomboa nchi yao. Uongozi wa sasa umefeli kabisa kutatua changamoto zinazowakumba,” akasema.

Seneta huyo pia alikosoa uzinduzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo na Serikali ya Jubilee kama Reli ya Kisasa (SGR), akisema haiwafaidi wananchi kwa vyovyote vile, ikizingatiwa kuwa baadhi ya maeneo inayopitia yanakumbwa na ukame.

“Miradi hii yote ni ya maana gani wakati tumeshindwa kutatua changamoto za kimsingi zinazowakumba Wakenya? Hii ni hadaa,” akasema.

Seneta huyo alizindua nia yake ya kuwania urais mnamo Desemba 27, alikosema atagombea nafasi hiyo kwa tiketi ya Chama cha Federal Party (FPK).

Alisema kuwa hatua yake inasukumwa na kusalitiwa kwa Wakenya na serikali za hapo awali tangu uhuru.

“Tunahitaji mabadiliko katika mkondo wetu wa kisiasa,” akasema, huku akiwaonya wapinzani wake kuwa waangalifu.