Wezi wachimba mashimo ardhini na kuiba katika maduka kumi

Na MAGDALENE WANJA

Imepakiwa - Monday, June 19  2017 at  06:50

Kwa Mukhtasari

WAFANYABIASHARA mjini Nakuru wanahofia mtindo mpya wa wizi ambapo wezi huchimba mashimo ardhini karibu na maduka na kutumia njia hiyo kuingia madukani.

 

Kufikia sasa, zaidi ya maduka 10 mengi yakiwa katika barabara ya Gusii, yamevunjwa na kuibiwa kupitia njia hiyo.

Wanabiashara hao walisimulia hofu kuwa  wizi utaendelea iwapo polisi hawatachukua hatua yoyote.

Hapo awali walikuwa wakiiba kwa kukata paa na tulipogundua tuliweka vyuma vizito na ndipo wakagundua njia hii mpya,”alisema mfanyabiashara ambaye tayari amepoteza mali ya zaidi ya Sh600,000.

Kulingana na wafanyabiashara hao, mtaro mkubwa ulionyuma ya maduka hayo umekuwa ukirahisisha njia ya wezi hao .

“Nilipata shimo nyuma ya duka langu ishara kwamba walijaribu kuingia usiku. Ijapokuwa hawakufaulu kuingia, nina hofu sana kwa sababu sijui nia nayo,” alisema Bi  Emma Wanjiku ambaye ameathiriwa na njia hiyo ya wizi.

Wafanya biashara hao wametaka usalama uimarishwe katika sehemu hiyo ya Gusii Road ambayo ina idadi kubwa ya vijana wanaofanya biashara.