Mwanahabari wa Sunday Nation akamatwa kwa kufichua siri za serikali

Na MWANDISHI WETU

Imepakiwa - Monday, June 19  2017 at  07:06

Kwa Mukhtasari

MWANAHABARI wa gazeti la Sunday Nation linalomilikiwa na kampuni ya Nation Media Group, Bw Walter Menya, Jumapili alikamatwa na polisi baada ya kuandika taarifa ya habari iliyofichua jinsi watumishi wa umma wanavyohusika katika kufadhili shughuli za Chama cha Jubilee.

 

Kupitia kwa Mhariri Mkuu Bw Mutuma Mathiu, Kampuni ya NMG ilihofia usalama wa mfanyakazi wake, ikizingatiwa kuwa Bw Menya huugua na alifungwa bila dawa zake.

Bw Menya alikamatwa asubuhi kwa madai kuwa alipokea hongo ili asiandike taarifa fulani, ingawa NMG ilishuku kukamatwa kwake kulitokana na taarifa hiyo ya watumishi wa umma iliyochapishwa jana.

Aliripoti kuwa watumishi watatu wa umma ni miongoni mwa maafisa waliosajiliwa kusimamia shirika la kampeni za Jubilee.

Hata hivyo, Inspekta Jenerali wa polisi Bw Joseph Boinnet, alidai Bw Menya alipokea hongo ya Sh35,000 kupitia kwa M-Pesa na alipokamatwa alikuwa anapokea Sh20,000.

Kukamatwa kwa Bw Menya kumezidisha rekodi mbaya ya uhusiano wa serikali ya Jubilee na wanahabari, ambao ulianza kudorora punde baada ya serikali kuingia mamlakani 2013.

Mbali na kutumia wingi wake bungeni kupitisha sheria za kukandamiza uanahabari nchini, ripoti ya shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch iliyotolewa Mei ilibainisha matukio ya kupigwa, kuuawa na kutishiwa kwa wanahabari yamezidi na yanahatarisha uwezo wa kufichua maovu ya viongozi.

Katika taarifa yake, Bw Menya alifichua kuwa shirika la Friends of Jubilee Foundation, limemsajili Kamishna wa Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru nchini Bw John Njiraini kama mwanachama wa bodi yake.

Wengine walio katika bodi hiyo, kulingana na upelelezi wa Bw Menya, ni Katibu wa Wizara ya Kawi Bw Joseph Njoroge. Wawili hawa wana mamlaka ya kuidhinisha utumizi wa fedha za shirika hilo.

Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na wageni walioalikwa pekee iligonga vichwa vya habari kwani zaidi ya Sh1 bilioni zilichangishwa kufadhili kampeni za Rais Uhuru Kenyatta.

Chama cha Wanahabari nchini (KUJ) kilitoa wito kwa wanahabari kuandamana leo kulalamikia kukamatwa kwa mwenzao.