Wafugaji wawataka wawaniaji kutia saini mkataba wa amani

Na TITUS OMINDE

Imepakiwa - Monday, July 17   2017 at  15:36

Kwa Mukhtasari

ZAIDI ya wachungaji 80 kutoka mjini Elodret wametaka wanasiasa ambao wanagombea nyadhifa mbalimbali wakati wa uchaguzi mkuu wa Agosti 8 kuweka saini katika mkataba wa kudumisha amani.

 

Mkataba huo ni kati ya wagombezi husika na wapiga kura.

Makuhani hao walisema hayo mtaani Langas wakati wa mkutano wa amani ambao uliwaleta pamoja zaidi wagombezi 10 ambao wanagombea viti mbalimbali.

Kwa pamoja waliwataka wafuasi wao kutowapigia kura wanasiasa ambao hawatatia saini katika mkataba huo hasa katika kaunti ya Uasin Gishu.

Wakiongozwa na askofu Paul Mwangi walisema mkataba huo unalazimisha kila mgombezi kutenga dakika 10 kwa kila mkutano wa kisiasa kuhubiri amani na kukariri kiapo cha kudumisha amani.

Miongoni mwa wagombezi ambao walihudhuria mkutano huo walikuwa ni wagombezi wa udiwani,ubunge, uakilishi wanawake na waakilishi wa wagombezi wa useneta na ugavana.

Akizungumza wakati wa mkutano huo mgombezi wa kiti cha uakilishi wanawake katika kaunti hiyo Bi Gladys Boss Shollei aliahidi kuheshimu mkataba huo.

 “Mkataba huu wapaswa kuheshimiwa na wnasiasa wote si hapa tu Uasin Gishu bali kote nchini,” alisema Bi Shollei

Bi Shollei aliwataka wakazi wa mtaa wa Langas ambao uliathiriwa pakubwa na ghasia za 2007 kujitenga na wanasiasa wachochezi wakati huu wa kampeini ya uchaguzi mkuu.