Wakati wa kuwaangamiza kabisa Al Shabaab umefika - Rais

Rais Uhuru Kenyatta

Rais Uhuru Kenyatta akihutubu awali. Picha/PSCU 

Na KALUME KAZUNGU

Imepakiwa - Monday, July 17  2017 at  18:04

Kwa Mukhtasari

RAIS Uhuru Kenyatta ametangaza vita vikali dhidi ya magaidi wa Al-Shabaab wanaohangaisha wakazi wa Lamu na hata kuua raia na maafisa wa usalama.

 

Akihutubu kwenye mkutano wa kampeni katika Bustani ya Uhuru, mjini Mpeketoni Jumatatu, Rais Kenyatta alisema wakati umefika wa serikali kukabiliana na magaidi na kuwamaliza humu nchini.

“Ikiwa wanadhani tutawabembeleza, basi wajue wamekosea. Tutakabiliana nao vivyo hivyo watakavyo. Haturudi nyuma,” akaonya rais.

Aliwataka wakazi wanaoishi kwenye vijiji ambavyo vimeathiriwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya Al-Shabaab katika kaunti hiyo ya Lamu wahame mara moja na kukimbilia maeneo salama ili kupisha vitengo vya polisi na jeshi kuendesha operesheni ya kuwamaliza wanamgambo hao.

“Ninaloomba ni nyinyi wananchi kushirikiana na vitengo vetu vya usalama na kutoa ripoti ili kusaidia katika kukabiliana na kuwamaliza magaidi hao. Kwa wale wanaoishi vijiji vya mashambani, mtoke huko ili mpishe walinda usalama wetu kuwasaka na kuwamaliza magaidi,” akasema Rais Kenyatta.

Alisema serikali imechoshwa na vitendo vya kikatili vinavyotekelezwa na magaidi wa Al-Shabaab ambao kila mara wamekuwa wakivamia na kuwaua ovyo raia wasio na hatia na polisi.

Wakati wa ziara hiyo, Rais Kenyatta aliwapa maskwota wa Mpeketoni jumla ya hatimiliki 800 za ardhi.

Alisema lengo la serikali ya Jubilee ni kuhakikisha kila Mkenya anafurahia haki yake ya kumiliki ardhi.

Rais pia aliwaomba wakazi wajitokeze kwa wingi ifikapo Agosti 8 ili kupigia kura Jubilee na kuiwezesha kuunda serikali ijayo.

“Muda mfupi ambao tumekuwa uongozini mimi na mwenzangu Ruto tumehakikisha Wakenya wako na stima, bili hospitalini kwa akina mama wajawazito hakuna, mradi wa reli ya kisasa unakamilika, elimu ya bure inafanikiwa, barabara ya Lamu kuelekea Garsen inatengenezwa na mengine mengi. Mtuchague kwa kipindi kingine ifikapo Agosti 8 ili tuweze kuunda serikali ijayo,” akasema.

Kwa upande wake, Naibu Rais William Ruto alidai kuwa viongozi wa muungano wa NASA wanaendeleza siasa za mgawanyiko na porojo.

Aliwataka Wakenya wasichague viongozi wa Upinzani,akidai kuwa hawana ajenda yoyote ya maana kwa nchi.

“Sisi ni serikali ya kusema na kutenda. Tayari tumetenda mengi na mnayaona. Je, mko tayari kuwapigia kura watu wa vitendawili na porojo ama mtatuchagua sisi ili tuendelee kuwahudumia?” akauliza.

“Wakati umefika wa nyinyi wakazi wa Mpeketoni na Lamu kuchagua uongozi bora, ambao ni wa Jubilee,” akasema Bw Ruto.