Kifo chawasubiri wanne waliopatwa na hatia ya mauaji

Na ALEX NJERU

Imepakiwa - Monday, July 17   2017 at  18:18

Kwa Mukhtasari

MAHAKAMA Kuu ya Chuka, Kaunti ya Tharaka-Nithi hapo Jumatatu iliwahukumu kifo wanaume wanne waliopatikana na hatia ya mauaji. 

 

Bw Wilfred Kioji, Jeff Murithi, Francis Murangiri na Silas Kimathi walishtakiwa kwa kosa la kuua Bw Mathew Gichuhi Nyaga mnamo Februari 13, 2016 katika kijiji cha Tunyai, kutokana na mgogoro wa ardhi na kuutupa mwili wake kwenye mto Mutonga. 

Katika hukumu yake, Jaji Robert Limo alisema mahakama hiyo imepokea ushahidi wa kutosha ili kuthibitisha kwamba kifo cha Bw Gichuhi kutoka kaunti ya Kirinyaga kilitokana na mgogoro wa ardhi kati yake na watuhumiwa ambao alikuwa amenunua kipande cha ardhi kutoka kwa marehemu baba yao. 

Alisema kuwa kulingana na ushahidi uliopokewa na korti hiyo, wanne hao walikuwa wakitishia marehemu kwa muda mrefu kwamba wangemuua iwapo asingeachana na shamba hilo.

Katika hukumu yake, Jaji Limo alisema ushahidi uliotolewa mahakamani na mashahidi kumi na mmoja ulidhihirisha wazi kuwa wanne hao walishirikiana kutekeleza kitendo hicho cha unyama.

Mmoja wa washukiwa, Bw Murangiri aliambia  korti kuwa siku hiyo, walipigana na marehemu na alipopiga kamsa na wenzake watatu kuja, mwendazake alikimbia na kijiangusha kwenye mto wa Mutonga.

Hata hivyo, kwa mujibu wa afisa wa uchunguzi, Bw Francis Ndirangu, kulikuwa na ishara ya mapambano nyumbani kwa marehemu na waliweza kufuata matone ya damu hadi kwenye mto huo ambapo mwili ulipatikana baada ya siku tatu. 

Dkt Justus Kitili, aliyefanya upasuaji wa mwili, aliambia koti kuwa mwili wa Bw Gichuhi ulikuwa na majeraha makubwa kichwani ambayo inaweza kuwa yalitokana na kupigwa na kifaa butu. 

Hakimu, aidha alisema kuwa kunauwezekano kitendo hicho cha unyama kilichangiwa na chifu wa Tunyai Bw Julius Mburio aliyetoa maneneo ya ukabila yaliyoashiria kuwa marehemu ambaye alikuwa mgeni eneo hilo alikuwa akinyakua mashamba ya wenyeji.