Wabunge 10 kutoka ngome ya Ruto wasema 'Raila Tosha'

Waziri Mkuu Raila Odinga

Mwaniaji urais wa NASA Raila Odinga. Picha/MAKTABA 

Na TITUS OMINDE na VALENTINE OBARA

Imepakiwa - Monday, July 17  2017 at  18:22

Kwa Mukhtasari

WABUNGE 10 waasi kutoka ngome ya Naibu Rais William Ruto, wamezindua kampeni ya kuupigia debe muungano wa NASA katika eneo la Rift Valley Kaskazini.

 

Wakiongozwa na Mbunge wa Chesumei Bw Elijah Lagat na aliyekuwa Mbunge wa Mosop, Bw David Koech, walizindua msafara wa kampeni za NASA mjini Eldoret, ambako ni ngome ya kisiasa ya Jubilee.

Waliapa kuanzisha kampeni za upinzani kutoka nyumba moja hadi nyingine huku wakilaumu serikali kwa kupuuza eneo hilo kimaendeleo.

“Wale wanaofikiria kuwa eneo hili ni ngome ya Jubilee wanaota. NASA imeimarika kwa sababu ya uongozi mbaya wa Jubilee,” akasema Bw Koech.

Jumatatu Bw Odinga alizuru Kaunti ya Homa Bay, na Jumanne amepangiwa kuelekeza kampeni zake eneo la Kibra, Kaunti ya Nairobi na duru zinasema anapanga kuzuru Rift Valley hivi karibuni.

Bw Koech aliendelea kusema kuwa wakazi wa Kaskazini mwa Rift Valley, hasa wakulima wanaunga mkono NASA kwa sababu ina manifesto nzuri inayozingatia mahitaji ya wakulima ikilinganishwa na Jubilee.

Mbunge wa zamani wa Emgwen, Bw Stephen Tarus, alisema wakulima wa eneo hilo wamechoshwa na Jubilee kwani imeshindwa kutetea haki zao.

“Tumeshangaa kuwa serikali imesaidia wakulima wa maeneo mengine nchini kwa kuwaondolea madeni waliyodaiwa na Shirika la Fedha za Kilimo huku wakulima wa Kaskazini mwa Rift Valley wakipuuzwa,” akasema Bw Tarus.

Wabunge wengine wa zamani waliojiunga na kampeni za NASA ni Francis Mutwol, John Cheruiyot, Jesse Mais, David Koech, Joseph Misoi, Peris Simam, Jenerali Mstaafu Augustine Cheruiyot na Diwani kutoka Kaunti ya Pokot Magharibi Bi Regina Nyiris.

Akiwa Homa Bay Jumatatu, Bw Odinga alitoa wito kwa vijana wawe katika mstari wa mbele kuunga mkono NASA kwa sababu kulingana naye, juhudi za upinzani zinalenga kuwaondolea matatizo waliyosababishiwa na serikali ya Jubilee.

“Hatima ya vijana wetu imevurugwa na Jubilee sawa na jinsi walivyovuruga uchumi, usimamizi wa miundomsingi, sekta ya afya na nyinginezo. Vijana wasijitambulishe kwa misingi ya kikabila bali kama Wakenya kwani ukabila hautawakomboa,” akasema Bw Odinga.

Alikuwa ameandamana na vinara wenzake Musalia Mudavadi wa chama cha Amani National Congress na Seneta wa Bungoma, Bw Moses Wetang’ula anayeongoza chama cha Ford Kenya, pamoja na viongozi mbalimbali wa kisiasa wa eneo hilo akiwemo Gavana wa Homa Bay, Bw Cyprian Awiti.

Bw Mudavadi na Bw Wetang’ula waliambia wakazi wa Homa Bay wahakikishe wamejitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi mkuu ili kumwezesha Bw Odinga kushinda urais.

Bw Mudavadi aliwaambia wafuasi wa NASA wasikubali kuhadaiwa na vitu tofauti wanavyopewa na wawakilishi wa serikali ili kuwavutia.

“Wale wanaotembea na mchele wakitumia magari ya serikali ili wafumbe watu macho eti ndipo wasimpigie Raila kura, nawaambia huo mchele ni ushuru wenu na hilo gari ni wewe umelipia kwa hivyo si msaada wanaowaletea,” akasema.