Raila, Uhuru na Moi kuhudhuria mazishi ya 'Total Man' Alhamisi

Nicholas Biwott

Marehemu Nicholas Biwott. Picha/BILLY MUTAI 

Na PHILEMON SUTER na WYCLIFFE KIPSANG

Imepakiwa - Monday, July 17  2017 at  18:29

Kwa Mukhtasari

MAANDALIZI ya mazishi ya waziri wa zamani Nicholas Biwott yameshika kasi nyumbani kwake katika kijiji cha Toot, Kaunti ya Elgeyo Marakwet.

 

Rais Uhuru Kenyatta naibu wake William Ruto, mwaniaji wa urais wa NASA Raila Odinga, mwenyekiti wa Kanu Gideon Moi ni miongoni mwa wageni wanaotarajiwa kuhudhuria mazishi hayo yatakayofanyika Alhamisi wiki hii, katika eneo la Keiyo Kusini.

Hafla ya mazishi itafanyika katika shule ya upili ya Maria Soti Girls iliyoko takribani kilomita 3 kutoka kijiji cha Toot.

Wageni wengine ni wafanyabiashara mashuhuri kama vile Manu Chandaria, Dkt Chris Kirubi na mabwanyenye wengineo kutoka sekta za huduma ya ndege na mafuta.

“Simba amefariki na tunatarajia kuwa simba wengine wadogo kwa wakubwa watahudhuria hafla ya mazishi yake,” akasema Bw Patrick Kibet, mkazi wa kijiji cha Toot.

Bintiye Biwott, Bi Esther Koimet ni miongoni mwa jamaa ambao wamefika kijijini Toot kufanya mipango ya mazishi.

Bi Koimet aliyekuwa ameandamana na jamaa wengine wa familia ya Biwott alizuru eneo la kaburi ambapo waziri huyo wa zamani atazikwa.

Bw Biwott ambaye alifahamika kwa jina la majazi, 'Total Man’ atazikwa karibu makaburi ya wazazi wake Mzee Cheserem Biwott na Mama Maria Soti.

Jana, serikali ya kitaifa na Kaunti ya Elgeyo-Marakwet ziliungana katika kukarabati barabara yenye urefu wa kilomita 10 kutoka eneo la Elgeyo hadi Toot.

Gavana Alex Tolgos aliwataka wakazi kujitokeza kwa wingi kumuaga Bw Biwott aliyekuwa waziri wakati wa utawala wa Rais Mstaafu Daniel arap Moi.

Gavana alisema serikali yake itaonyesha heshima kuita moja barabara jina la Mzee Biwott.