http://www.swahilihub.com/image/view/-/3452290/medRes/1487914/-/rbutnr/-/PAS.jpg

 

Wawaniaji wanawake waililia serikali iwape usalama

Bi Esther Passaris

Mwakilishi Mwanamke wa kaunti ya Nairobi Bi Esther Passaris. Picha/ HISANI 

Na BRIAN MOSETI

Imepakiwa - Monday, July 17  2017 at  18:38

Kwa Mukhtasari

WAGOMBEAJI wanawake wa nafasi za kisiasa wamelalamika kwamba hawana ulinzi wa kutosha, hali inayowazuia kufanya kampeni katika baadhi ya maeneo hasa yanayokisiwa kuwa si salama.

 

Baadhi ya wagombeaji hao waliohudhuria mkutano wa wadau ulioandaliwa na Shirika la Mawakili wa Kike (FIDA) katika hoteli ya Nairobi, walisema wamekuwa wakikutana na umati usiowafurahia, wao wenyewe na wafuasi wao kuzuiwa kufika maeneo ya kampeni na hata kupigwa.

Walisema kuwa wanaume wengi wanaoshindana nao wanapewa ulinzi na hata wana walinzi wao wa kibinafsi ilhali wao hawana.

“Tuliahidiwa kuwa tutapewa ulinzi lakini bado hatujauona kwani hatuwezi kwenda maeneo mengine kwa sababu tunaogopa,” akasema Bi Winnie Kaburu , ambaye ndiye mwanamke pekee anayeshindania ugavana na wanaume sita katika Kaunti ya Meru.

“Kuna dhana kuwa mwanamke anaposhindana na wanaume huenda kukawa na ghasia na kwamba mwanamke akishindana na wingine hakutakuwa na ghasia.

Lakini dhana hiyo haina msingi kwa sababu wafuasi wanaweza kuchochewa kufanya lolote,” akasema Bi Esther Passaris, anayewania kiti cha Mwakilishi Mwanamke Kaunti ya Nairobi.

Alisema kuwa wanawake wote wanaogombea kiti hicho hawajapewa ulinzi wowote.

Hata hivyo, Msemaji wa Polisi, Bw Charles Owino, alisema walinzi wa kibinafsi wanapewa wanaogombea urais pekee na si wagombeaji wa nafasi zingine.

“Tumekuwa na mazungumzo haya na wagombeaji wa kike lakini haikuwezekana kumpatia kila mmoja mlinzi kwa kuwa hatuna uwezo huo,” akasema Bw Owino na kuongeza kuwa walikuwa wamefanya mipango na wakuu wote wa polisi kuhakikisha kuwa kuna usalama katika maeneo yote ya kampeni.

Alifafanua pia kuwa viongozi waliopo, magavana, maseneta, wabunge na Wawakilishi Wanawake tayari wana walinzi waliopewa kabla ya kipindi cha kampeni.

Mkutano wa jana ulilenga kuhakikisha kuwa wanawake wanapata ushindi katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti, na shirika hilo lilitangaza kuwa litatoa huduma zake bila malipo kwa wanawake ambao watataka kupinga matokeo ya uchaguzi baada ya uchaguzi kumalizika.

“Fida itatoa huduma zake bila malipo, ambazo zitajumuisha wakili, kulipa ada zote za mahakama na kutoa usalama kwa wanaouhitaji,” akasema Mwenyekiti wa FIDA, Bi Josephine Mongare.

Hata hivyo, Bi Truphena Estambale wa Jopo la Kutatua Mizozo ya Vyama vya Kisiasa, alisema ikilinganishwa na siku za nyuma, wanawake wameanza kujitokeza kupinga maamuzi ya vyama.

Alitoa mfano wa kati ya Aprili na Juni mwaka huu, ambapo kesi 300 ziliwasilishwa kwa jopo, 40 zikiwa kutoka kwa wanawake. Suala kuu alisema ni majina yao kukosekana katika sajili za vyama ama watu wengine kudai ndio wao.

Kadhalika, mkurugenzi wa huduma za kisheria katika Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Bi Praxedes Tororey aliwauliza wanawake kujitokeza na kulalamika ikiwa kampeni zao zitaingiliwa kati.