Aliyemkata mpenziwe mkono asukumwa ndani maisha

Na PIU MAUNDU

Imepakiwa - Thursday, December 7  2017 at  15:39

Kwa Muhtasari

MWANAMUME aliyemkata mikono mpenzi wake alipotisha kumuacha miaka miwili iliyopita Jumatano alifungwa jela maisha.

 

Reuben Kivuva, 35, anayefahamika kwa jina maarufu Cameroon, alimkata mikono Bi Judith Muendi Desemba 13, 2015 katika chumba walichokuwa wakiishi mjini Emali, kaunti ya Makueni.

Alishtakiwa katika mahakama ya Makindu kwa kujaribu kumuua Bi Muendi, 28 na jana, Hakimu Mkuu Mkazi Gerald Mutiso, alimpata na hatia.

“Nimezingatia kilio cha mshtakiwa kwamba ni baba ya watoto watatu na mume wa mke anayeugua kifafa na mama yake ni mgonjwa,” alisema Bw Mutiso akisoma hukumu yake.

“Pia, nimezingatia ripoti ya hali ya maisha ya mwathiriwa ambaye kwa sasa anamtegemea mama yake kumuosha, kumvisha na kumpikia. Ukatili ambao mshtakiwa alimtendea mwanamke asiyeweza kujilinda unashtua,” alisema hakimu.

Hakimu alisema mshtakiwa alimkata mikono mwanamke huyo kwa sababu alitaka kumuacha baada ya kugundua alikuwa na mke mwingine.

Alisema mahakama ilithibitishiwa kuwa Kivuva alitaka kumuua mpenzi wake na alifaa kupata adhabu kali.

Wakili wa mshtakiwa Francis Mwangangi, alikuwa amefahamisha mahakama kwamba, mshtakiwa alitaka kuuza pikipiki yake yenye thamani ya Sh150,000 kumfidia Muendi na familia yake.

Hata hivyo, mahakama ilisema kiwango hicho ni kidogo mno na ikaagiza pikipiki hiyo ikabidhiwe mwanamke huyo kuitumia.