http://www.swahilihub.com/image/view/-/4567604/medRes/1976748/-/uqb8ytz/-/sh+pic.jpg

 

Wanakijiji wagoma kupokea madarasa ya shule ya msingi

 

Na Anthony Mayunga

Imepakiwa - Friday, May 18  2018 at  08:35

Kwa Mukhtasari

Ofisi ya Hlamashauri ya Wilaya ya Serengeti imezuia malipo ya zaidi ya Sh 6 milioni

 

 

Serengeti. Wakazi wa Kijiji cha Nyanungu wilayani hapa, Mkoa wa Mara wamekataa kupokea vyumba vitatu vya madarasa vilivyojengwa katika Shule ya Msingi Nyanungu baada ya kubaini yapo chini ya kiwango.

Kutokana na hali hiyo, wameomba timu maalumu ya wakaguzi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kukagua majengo hayo kabla malipo ya mwisho kufanyika ili kulinda fedha na masilahi ya umma.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya kijiji hicho, Mwita Sibora alitaja miongoni mwa kasoro zilizobainika ni vyumba hivyo kuezekwa kwa mabati ya geji 30 badala ya 28 iliyoko kwenye mkataba wa ujenzi.

“Tayari tumezuia malipo yaliyobaki hadi uchunguzi ufanyike na hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi ya wote waliotumia vibaya fedha za umma,” alisema Sibora.

Alifafanua kuwa kutokana na vyumba hivyo kukosa ubora, kikao cha wazazi kilichoitishwa kujadili suala hilo kiliazimia wanafunzi wasitumie vyumba hivyo.

Hali hiyo imesababisha wanafunzi zaidi ya 500 wa shule hiyo kubanana kwenye vyumba vinne vilivyopo.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Nyanungu, Mwita Ibaba alijivua lawama kuhusu uongozi wake kuidhinisha malipo ambayo wananchi waliyazuia, akisema uamuzi huo ulitokana na ushauri wa wataalamu wa halmashauri waliopitisha ubora wa mradi huo.

Msimamizi wa mradi huo, Boni Manga alikiri madarasa hayo kuezekwa kwa mabati ya geji 30 na kuahidi kuyaezua na kupaua upya ya geji 28.

“Tayari nimepokea malipo ya Sh12 milioni kati ya fedha zote; nitatumia sehemu ya fedha hizo kufanya marekebisho ya kasoro zilizobainika,” alisema Manga.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Juma Hamsini alisema ofisi yake imezuia malipo ya zaidi ya Sh6 milioni yaliyosalia hadi hapo timu ya wataalamu itakapokagua na kuridhika na ubora wa vyumba hivyo kulingana na thamani halisi ya fedha.