Afisi za IEBC zihamishiwe Bomas - Wabunge wa Jubilee

Na CHARLES WASONGA

Imepakiwa - Thursday, October 12  2017 at  20:29

Kwa Mukhtasari

WABUNGE wa Jubilee kutoka Nairobi wameitaka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuhamisha makao yake kutoka katikati mwa jiji hadi ukumbi wa Bomas

 

Wakiongozwa na Mbunge wa Starehe Charles Njagua, almaarufu 'Jaguar' wabunge hao sita walisema uwepo wa afisi hizo katika jumba la Anniversary imekuwa chanzo wa usumbufu kwa wafanyabiashara maeneo hayo kutokana na maandamano ya wafuasiwa NASA.

"Wafanyabiashara wa katikati mwa jiji wamenilalamikia kwamba maandamano ya kila mara hasa karibu na jumba la Anniversary yanaathiri biashara zao. Hii ndio maana leo asubuhi nimeiandikia IEBC nikiiomba kuhamisha afisa zake hadi Bomas," akasema.

Kauli yake iliungwa mkono na wenzake, Yusuf Hassan (Kamukunji), Nixon Korir (Langata), Benjamin Mwangi (Embakasi ya Kati), Wahinya Ndirangu (Roysambu) na George Theuri (Embakasi Magharibi).

Wabunge hao walilaani maandamano yanayoendeshwa na wafuasi kila wiki katikati mwa jiji la Nairobi wakisema yanaathiri shughuli za kibiashara kuvutia wahalifu. Ndiposa wakaunga mkono hatua ya Kaimu Waziri wa Usalama Fred Matiang'i wa kuzima maandamano katika miji ya Nairobi, Kisumu na Mombasa.

"Kile tulichoshuhudia katikati mwa jiji la Nairobi jana (Jumanne) hakikuwa maandamano bali visa vya ujambazi ambapo wananchi walikuwa wakiporwa hadhara, maduka yakivunjwa na magari kugongwa mawe. Hii sio maana ya maandamano kulingana na kipengee cha 37 cha Katiba," akasema Bw Yusuf.