Afueni kwa mkurugenzi aliyekaidi kufika kortini

Na BENSON MATHEKA

Imepakiwa - Monday, March 20   2017 at  14:46

Kwa Mukhtasari

ALIYEKUWA mkurugenzi wa shirika la Shelter Afrique Jumatatu alinusurika kusukumwa rumande kwa kukosa kufika kortini alivyoagizwa na Mahakama. 

 

Hakimu Mkuu wa Kibera Joyce Gandani aliondoa kibali cha kumkamata Louis Rodgers Ouadji,  raia wa Cameroon alichotoa mwezi uliopita alipofika korti mwezi jana.

Ouadji aliyeandamana na familia yake korti alisema alisahau tarehe aliyotakiwa kufika kortini.

"Mheshimiwa, nilisahau tarehe hiyo na ndio maana nimejileta kortini bila kushurutishwa ili kuonyeshwa heshima kwa mahakama hii, "alisema.  Aliambia mahakama kwamba amekuwa akishirikiana na korti ambayo umekuwa ikimruhusu kuondoka nchini kwa ziara za kikazi. Bi Gandani aliondoa kibali cha kumkamata lakini akamuonya kuzingatia tarehe anazopewa na Mahakama. 

Katika kesi hiyo amekanusha kwamba alishirikiana na watu wengine ambao hawakuwa mahakamani, kupora Bw Peter George Ndungu,vifaa vya ujenzi vya thamani ya Sh355,050 wakijihami kwa panga na rungu.

Kulingana na shtaka ilidaiwa alitenda kosa hilo Novemba 2 2015, ambapo walitumia nguvu kamili dhidi Bw Ndungu aliyekuwa akisimamia ujenzi kwenye ploti inayozozaniwa. 

Mahakama iliambiwa kuna kesi katika mahakama kuu ambapo mshtakiwa anataka korti iamue mmiliki halisi wa ardhi hiyo. Bw Ouadji alisema japo kesi hiyo ilikuwa ikisikilizwa na Hakimu aliyepandishwa cheo kuwa jaji, anataka iendelee ilipofikia.

Kesi itatajwa Mei 8 mwaka huu.