http://www.swahilihub.com/image/view/-/2338406/medRes/647606/-/oabmfnz/-/MPAlfredKeter.jpg

 

Alfred Keter aadhibiwa kwa kuikaidi Jubilee

Nandi Hills Alfred Keter

Mbunge wa Nandi Hills Alfred Keter akihutubu awali. Picha/JARED NYATAYA 

Na  CHARLES WASONGA

Imepakiwa - Wednesday, December 20  2017 at  20:34

Kwa Muhtasari

MBUNGE wa Nandi Hills Alfred Keter ni miongoni mwa wabunge watatu ambao wameondolewa kutoka kamati za bunge kwa kushindana na wenzao ambao walikuwa wamependekezwa na chama cha Jubilee.

 

Wengine ni Mbunge wa Marakwet Mashariki Kangogo Bowen na mwenzake wa Emgwen Bw Alex Kosgey.

Bw Keter ambaye ni mbunge mbishani alikaidi msimamo wa Jubilee kwa kuwania wadhifa wa uenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Leba na kumshinda Mbunge wa Bura Ali Wario ambaye juzi alipendekwa katika mkutano wa kundi la wabunge wa Jubilee ulioongozwa na Rais Uhuru Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi.

Bw Keter alipata kura 11 huku Wario akipata kura 6 pekee.

Naye Bw Kagongo alishindana na Mbunge wa Ijara Sophia Abdi katika kinyang'anyiro cha naibu uenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Mazingira.

Bw Kosgey naye alikaidi msimamo wa chama na kushindana na Mbunge wa Kieni katika uchaguzi wa mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Biashara, Viwanda na Vyama vya Ushirika. 

Hata hivyo, Bw Kega aliibuka mshindi kwa kupata kura 11 huku Kosgey akapata kura tano. Msimamo wa Jubilee ulikuwa ni kwamba Bw Kega alifaa kuchaguliwa bila kupinga.

"Kwa kwa mujibu wa mamlaka yangu na kwa kuzingatia sheria za bunge nimewaonda wabunge hawa watatu, Alfred Keter, Kagongo Bowen na Alex Kosgey kutoka kamati walizoteuliwa kuhudumu.

Hatua hiyo imechukuliwa kwa sababu watatu hao walikwenda kinyume na msimamo wa chama; hatua ambayo inafasiriwa kuwa utovu wa nidhamu," akasema kiranja wa wengi Benjamin Washiali kwenye barua aliyomtumia karani wa bunge Michael Sialai.

Nakala ya barua hiyo ilitumwa kwa kwa Kiongozi wa walio wengi bungeni Aden Dauale, na Spika Justin Muturi.