Askari jela watisha kugoma wasipolipwa Sh10,000 kama wenzao wa AP

Na VALENTINE OBARA

Imepakiwa - Monday, June 19  2017 at  07:39

Kwa Mukhtasari

ASKARI jela wametishia kuanza mgomo baridi Jumatatu, kama hawatalipwa marupurupu ya Sh10,000 kila mmoja.

 

Tishio hilo lilitolewa Jumapili kufuatia ripoti kuwa polisi wa kawaida na wale wa utawala walilipwa marupurupu ya kiasi hicho kwa kusimamia kura za mchujo wa vyama zilizofanyika Aprili.

Afisa anayehudumu katika gereza kuu la Kamiti lililo Kaunti ya Kiambu, ambaye aliomba asitajwe jina, alisema serikali imeonyesha ubaguzi kwa kulipa maafisa wa vitengo vingine na kuacha wengine ambao pia walishiriki kutoa ulinzi katika michujo kitaifa.

Hata hivyo, mkuu wa gereza hilo Bw Henry Kisingu, alisema askari hao tayari walifahamishwa watapewa marupurupu hayo sawa na wenzao.

“Niliwaonyesha barua na hata kubandika kwenye ubao wa notisi. Tatizo lilitokea kwamba marupurupu hayo yalitolewa wakati mishahara yao tayari ilikuwa imepagwa,” akasema.

Afisa aliyezungumza na 'Taifa Leo’ alisema waliosimamia michujo walikuwa kazini sawa na wengine ambao walibaki vituoni kufanya kazi zingine, hivyo basi kama marupurupu yanalipwa inastahili kuwa kwa polisi wote.

“Hatua hii italeta mgawanyiko katika idara ya polisi. Isitoshe, polisi wengine pia walikuwa kazini. Mbona walipe baadhi na kuwaacha wengine?” akasema.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, ilifichuka polisi walipokea Sh10,000 zaidi kwenye mishahara yao ya Juni.

Ilisemekana walipouliza pesa hizo ni za nini, waliandikiwa barua kutoka kwa makao makuu ya polisi kuambiwa ni za jinsi walivyotoa usalama wa hali ya juu wakati wa mchujo na wanavyozidi kutoa usalama wakati wa kampeni za kisiasa.

Vikosi vingine ambayo vilihusika katika shughuli hiyo ni maafisa wa Huduma za Vijana kwa Taifa (NYS), Huduma za Wanyamapori nchini (KWS) na wale wa kulinda misitu.