BURIANI TOO: Mwana wa kisiasa wa Moi afariki

Mark Too

Mbunge wa zamani Bw Mark Too. Picha/MAKTABA 

Na BENSON MATHEKA na BARNABAS BII

Imepakiwa - Sunday, January 1  2017 at  13:59

Kwa Mukhtasari

ALIYEKUWA mbunge maalumu mwenye ushawishi mkubwa wakati wa utawala wa chama cha Kanu Mark Too alifariki Jumamosi akitibiwa katika hospitali moja mjini Eldoret.

 

Bw Too aliyekuwa mwandani wa karibu wa Rais Mstaafu Daniel Moi alikimbizwa katika hospitali ya St Lukes mjini Eldoret mwendo wa saa tisa alasiri baada ya kupata matatizo ya kiafya.

Bw Too aliyefahamika kama Bw Dawa kutokana na ushawishi wake katika siasa na biashara pia alikuwa mfanyabiashara tajiri na mkulima shupavu.

Ushawishi wake katika siasa katika utawala wa Kanu ulifanya wengi kumpachika jina la mwana wa kisiasa wa Rais Moi.

Jumamosi, familia yake ikiongozwa na mkewe Mary Too ilikusanyika katika hospitali ya St Lukes baada ya kupata habari kuhusu kifo chake.

Ilisemekana kuwa mwanasiasa huyo alipelekwa katika hospitali hiyo baada ya kuugua ghafla akiwa nyumbani kwake Eldoret.

Japo alikuwa mtetezi sugu wa chama cha Kanu wakati wa utawala wa Rais Moi, alihama chama hicho 2011 na kujiunga na naibu rais William Ruto aliyekuwa akiongoza chama cha United Republican Party.

Wadadisi wa kisiasa walisema huenda alichukua hatua hiyo ili kulinda maslahi yake ya kibiashara kutokana na umaarufu wa Bw Ruto kuimarika.

Akiwa mbunge maalumu enzi za utawala wa Kanu, Bw Too aliteuliwa waziri msaidizi katika ofisi ya rais. Kwenye kitabu chake Flame of Freedom, aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga anamtaja Bw Too kama mwanasiasa aliyekuwa na ushawishi mkubwa zaidi katika utawala wa Moi.

Anasema wakati mmoja alipokuwa katika juhudi za kuunganisha chama alichoongoza cha NDP na Kanu, alishangaa Rais Moi alipomwambia angewasiliana naye kupitia Bw Too.

“Nilishangaa kwamba ni Bw Too aliyekuwa wakala kati yangu na Rais Moi licha ya kuwa mipango ya kukutana naye ilikuwa imefanywa na Bw Reuben Chesire,” Bw Raila anaandika katika kitabu chake.

Ucheshi

Licha ya kuwa na ushawishi wa kisiasa, Bw Too alifahamika kwa kuendesha siasa zake kwa ucheshi ambao ulimwezesha kushirikiana na wanasiasa tofauti.

Miongoni mwa kampuni alizomiliki ni Lonrho East Afrika ambayo alikuwa mwenyekiti kwa miaka mingi.

Bw Too alikuwa miongoni mwa watu waliotetea maskwota katika msitu wa Mau dhidi ya kufurushwa na serikali ya muungano 2009.

Kufariki kwake kunajiri miaka mitatu baada ya mshirika mwingine wa Rais Moi eneo la Kaskazini mwa bonde la ufa Ezekiel Barngertuny kuaga dunia.