Babu Owino sasa aililia mahakama imhurumie

Babu Owino

MBUNGE wa Embakasi mashariki Paul Ongili almaarufu Babu Owino alipofikishwa kortini Alhamisi. PICHA/ RICHARD MUNGUTI 

Na RICHARD MUNGUTI

Imepakiwa - Thursday, October 12  2017 at  20:50

Kwa Mukhtasari

MBUNGE wa Embakasi Mashariki Paul Ongili almaarufu Babu Owino Alhamisi aliiomba mahakama kuu imkubalie awasilishe ushahidi katika kesi ya kupinga ushindi wake.

 

Alimsihi Jaji Joseph Sergon asiharamishe uchaguzi wake kwa vile hakuchelea kwa kupenda kujibu madai ya kesi dhidi yake.

Alisema hajakiri kwamba hakushinda kwa njia isiyo halali bali kama anavyodai aliyekuwa mwaniaji wa kiti hicho kwa tikiti ya chama cha Jubilee Francis Wambugu Mureithi.

Wakili Jackson Awele anayemwakilisha Babu Owino alimsihi Jaji Sergon amkubalie mbunge huyo awasilishe  ushahidi na majibu kwa vile hakuchelewa kuuwsilisha ushahidi kwa utukutu mbali alifahamishwa kama wakati umeenda na msaidizi wake kwamba kulikuwa na arifa iliyochapishwa katika magazeti ikitangaza kesi hiyo na kumtaka awasilishe majibu.

Tayari ameandikisha ushahidi kutoka kwa watu 32. “Naomba hii korti inihurumie niwasilishe ushahidi wangu niutetee ushindi wangu,” alirai Babu Owino

Kesi ya kupinga ushindi wa Babu Owino iliwasilishwa kortini na mwaniaji wa kiti hicho kwa tikiti ya chama cha Jubilee Bw Francis Mureithi.

Bw Mureithi , kupitia kwa wakili Ham Lagat aliomba mahakama iharamishe uchaguzi wa Babu Owino kwa vile hakujibu madai kwamba hakushinda kiti hicho kwa njia iliyowazi.

“Naomba hii mahakama itangaze kwamba Babu Owino amekiri kwamba hakushinda kwa njia halali,” alisema Bw Lagat.

Bw Lagat alisema Babu Owino alichelewa kwa muda wa siku 12 kuwasilisha majibu.

Pia alisema afisa aliyesimamia uchaguzi katika eneo hilo la Embakasi Mashariki Bw Nicholas Buttuk hakuwasilisha ushahidi katika muda unaofaa.

Bw Awele alikiri kwamba mshtakiwa aliwasilisha ushahidi kama amechelewa kwa muda wa siku tano.

“Babu Owino hakuona tangazo lililowekwa katika gazeti likisimulia kuhusu kesi ya kupinga ushindi wake. Alijulishwa mnamo Septemba 11 na keshoye akawasilisha majibu,” alisema Bw Awele.

Jaji Sergon atatoa uamuzi Oktoba 13 ikiwa ataharamisha uchaguzi wa Babu Owino au la.