Benki ya Dunia yaonya Kenya kuhusu mzigo wa deni la Sh3.8 trilioni

Na  BERNARDINE MUTANU

Imepakiwa - Thursday, April 20  2017 at  18:37

Kwa Mukhtasari

BENKI ya Dunia imeonya Kenya kuhusiana  na mzigo mkubwa wa deni ambao kwa sasa ni zaidi ya trilioni tatu.

 

Benki hiyo ilionya kuwa huenda deni hilo likawa na athari mbaya za kiuchumi nchini. Deni hilo limeongezwa na idadi kubwa ya mikopo iliyochukuliwa na serikali kufadhili miradi ya maendeleo.

Mtaalamu wa uchumi wa Benki ya Dunia anayesimamia eneo la Afrika Albert Zeufack na  afisa mkuu wa masuala ya uchumi wa benki hiyo Punam Chuhan-Pole walionya serikali kuwa lazima iweke katika mizani miradi ya maendeleo na athari za kukopa zaidi ya viwango vya mwisho.

Kwa muda wa miaka minne, Kenya imekopa mabilioni ya fedha kufadhili miundo msingi ikiwemo ni pamoja na ujenzi wa reli ya SGR na uzinduzi wa miradi ya kawi na ujenzi wa barabara.

Makadirio ya hivi majuzi yanaonyesha kuwa huenda mikopo ikalemea mapato ya ndani ya nchi kwa asilimia 60 ya mapato hayo.

Mwishoni mwa 2016, deni hilo lilikuwa asilimia 51.50 ya mapato yote ya Kenya kulingana na Hazina ya Fedha.

Kufikia sasa, mzigo wa deni nchini ni trilioni 3.827.