http://www.swahilihub.com/image/view/-/4137076/medRes/1779078/-/4w64c1/-/tt.jpg

 

Berardelli aachiliwa

Claudio Berardelli

Kocha wa kimataifa Claudio Berardelli (kulia), Dkt Stephen Tanui na Kocha Daniel Kiplangat wakiwa kizimbani Alhamisi walipoachiliwa na hakimu Kennedy Cheruiyot kwa kosa la kumpa bingwa wa mbio za Marathon Rita Jeptoo dawa za kututumua misuli 2015. Picha/ RICHARD MUNGUTI 

Na RICHARD MUNGUTI

Imepakiwa - Thursday, October 12  2017 at  19:19

Kwa Mukhtasari

KOCHA wa kimataifa wa riadha Claudio Berardelli aliyeshtakiwa kwa kumpa bingwa wa mbio za marathon ulimwenguni Rita Jeptoo dawa za kututumua misuli alichiliwa Alhamisi na Mahakama Kuu ya Milimani Nairobi.

 

Bw Berardelli , ambaye ni raia wa Italia mwenye umri wa miaka 38 aliachiliwa pamoja na kocha mwingine Daniel Cheribo Kiplangat na Dkt Stephen Tanui almaarufu Kalya walioshtakiwa pamoja kwa kufanya njama za kumharibia taaluma bingwa huyo wa mbio za marathoni.

Hakimu mwandamizi Bw Kennedy Cheruiyot alisema kati ya mashahidi 12 walioitwa na upande wa mashtaka “hawakuthibitisha jinsi watatu hao walifanya njama za kumpa Jeptoo dawa hizo zilizopigwa marufuku za kuongeza wanariadha nguvu wanapowania mbio.”

Hata hivyo Bw Cheruiyot alimpata na hatia Dkt Tanui ya kuuza dawa bila leseni mjini Kapsabet.

“Ninyi wawili Berardelli na Kiplangat mko huru kabisa.Tokeni mwende zenu kabisa. Korti imewaachilia,” alisema Bw Cheruiyot.

Vile vile , hakimu aliamuru dhamana ya Sh200,000 waliyokuwa wamelipa Berardelli na Kiplang'at warudishiwe pamoja na hati za kusafiri.

“Wewe utaanza kujitetea Novemba 10,” Bw Cheruiyot alimweleza Dr Tanui aliyempata na hatia katika mashtaka mawili ya kutokuwa na leseni ya kuuza dawa.

Watatu hawa walikuwa wameshtakiwa kufanya njama za kumharibia taaluma Bi Jeptoo.

Berardelli alifikishwa kortini Julai 2015.

Jeptoo amepigwa marufuku miaka minne kushiriki katika mbio na chama cha wanariadha nchini na pia na shirikisho la riadha  ulimwenguni IAAF.