http://www.swahilihub.com/image/view/-/3509996/medRes/1062470/-/9m172y/-/DNYATTA1407Y.jpg

 

Nyenze alisaidia NASA kupata mwaniaji mmoja wa urais - John Mbadi

Wabunge wa Ukambani

Marehemu Francis Nyenze (pili kutoka kushoto) na wabunge wengine wakihutubia wanahabari awali. Picha/DIANA NGILA 

Na CHARLES WASONGA

Imepakiwa - Wednesday, December 6  2017 at  19:32

Kwa Muhtasari

WABUNGE Jumatano walimtaja marehemu Mbunge wa Kitui Magharibi Francis Nyenze kama kiongozi mkomavu, mwadilifu na aliyechangia pakubwa ufanisi wa shughuli za bunge hata nyakati za mzozo.

 

Wakiongozwa na Spika wa Justin Muturi walisema mchango wake bungeni na Kenya kwa jumla kazi ambayo alianza kwa ukakamavu alipoingia kwa mara ya kwanza bunge mnamo 1997.

"Ni huzuni kuu kwetu kama wanachama wa asasi ya bunge kumpoteza mwenzetu Bw Francis Nyenze ambaye alifariki leo adhuhuri katika Nairobi Hospital baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Alikuwa kiongozi shupavu na mnyenyekevu, mpatanishi na ambaye mchango wake utakoswa zaidi katika bunge hilo na Kenya kwa jumla," akasema Bw Muturi.

"Kwa niaba yangu, familia yangu na bunge hili ningependa kuhakikkishia familia ya mwendazake kwamba tutafanya kila tuwezalo kusaidia familia yake wakati huu mgumu," akaeleza.

Nao kiongozi wa wengine Aden Duale na mwenzake wa wachache John Mbadi walimiminia ambaye alichangia pakubwa kuwezesha bunge la 11 kupitisha zaidi ya miswada 118. Marehemu Nyenze alikuwa kiongozi wa wachache katika bunge hilo.

"Kwa kweli Nyenze alikuwa kiongozi mpole lakini mkomavu. Hakuwa kiongozi aliyependa makabiliano; sifa ambayo wakati mwingi ilipelekea baadhi ya wenzake katika upinzani kumsawiri kama msaliti," akasema Bw Duale ambaye pia ni Mbunge wa Garissa Mjini (Jubilee).

Naye Bw Mbadi alimtaja marehemu kama kiongozi mpatanishi na aliyesaidia muungano wa NASA kuweza kupata mgombeaji mmoja wa urais katika uchaguzi mkuu wa Agosti 8 mwaka huu.

"Ama kwa marehemu alikuwa ni kiongozi mwenye uzoefu mkubwa sana katika uongozi wetu kama upinzani. Ni mtangulizi wangu katika wadhifa huu ninaoushikilia sasa. Chini ya uongozi wake nilikuwa nikimrejelea kama "Waziri Nyenze" huku akinirejelea kama 'kiongozi'", akaeleza mbunge huyo wa Suba.

Wabunge wengine waliomwomboleza Nyenze ni Chris Wamalwa (Kiminini), Bi Cecily Mbarire (Mbunge Maalum), Katoo Ole Metito (Kajiado Kusini), Makali Mulu (Kitui ya Kati), Benjamin Washiali (Mumias Mashariki), Nelson Koech (Belgut) na Olago Aluoch (Kisumu Magharibi).