http://www.swahilihub.com/image/view/-/3068502/medRes/1250744/-/6et1rm/-/snKAIKAI%252810%2529.jpg

 

Canada yakashifu Kenya kwa kutesa Miguna Miguna

Miguna Miguna

Wakili mashuhuri Bw Miguna Miguna kwenye mahojiano na mwanahabari. Picha/MAKTABA 

Na MAUREEN KAKAH

Imepakiwa - Friday, February 9  2018 at  07:20

Kwa Muhtasari

Serikali ya Canada imeikashifu serikali ya Kenya kwa kumtesa raia wake Miguna Miguna na kutaka hakikisho kwamba hakuna raia wake mwingine ambaye atadhulumiwa kwa kuishi ama kufanya kazi nchini Kenya.

 

SERIKALI ya Canada imeikashifu serikali ya Kenya kwa kumtesa raia wake Miguna Miguna na kutaka hakikisho kwamba hakuna raia wake mwingine ambaye atadhulumiwa kwa kuishi ama kufanya kazi nchini Kenya.

Kwenye barua iliyoandikia Wizara ya Mashauri ya Kigeni, Ubalozi wa Canada nchini ulisema kwamba umesikitishwa pakubwa na jinsi Bw Miguna alidhulumiwa na polisi.

Aidha, ubalozi huo ulilalama kwamba haukufahamishwa kuhusu kukamatwa kwake.

Mbali na hayo, ulilalama kwamba wawakilishi wake hawakuruhusiwa kumwona wakati walienda kumtembelea katika seli.

Hivyo basi, uliitaja hatua hiyo kama ukiukaji wa Mkataba wa Vienna, unaotoa mwongozo kuhusu taratibu zinazopaswa kufuatwa katika kuwakabili raia wa mataifa ya kigeni.

“Ubalozi wa Canada umeshangazwa sana na vitendo vya kuizuia serikali ya Canada kufuatilia hali ya raia wake. Kwa hivyo, unataka hakikisho kwamba hakutakuwa na vikwazo kama hivyo katika siku za usoni,” ikasema barua hiyo.

Canada ilieleza kwamba iliomba kibali cha kumtembelea Bw Miguna katika Kituo cha Polisi cha Lari mnamo Februari 4, ila ikanyimwa kibali.

Ilisema kwamba wakati maafisa wake walipofika katika kituo hicho, hawakupewa habari zozote kuhusu Bw Miguna, wala kuruhusiwa kumwona, hasa baada ya kuibuka madi kuwa hali yake ya afya haikuwa nzuri.

Walikuwa wakitaka kujua ikiwa angali anazuiliwa katika kituo hicho, au alikuwa ashahamishwa. Kulikuwa na habari kwamba Bw Miguna anaugua ugonjwa wa mapafu.

Ubalozi pia ulilalama kwamba juhudi za maafisa wake kuwapigia simu polisi hazikufua dafu, kwani walishindwa kabisa

Kwa hayo, ulisema kwamba lazima haki za Bw Miguna ziheshimiwe, kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

“Serikali ya Canada inataka uchunguzi kamili kufanywa kubainisha ikiwa raia wake (Miguna) alidhulumiwa na ni kwa kiwango kipi. Tunataka matokeo ya uchunguzi huo utakapokamilika,” ikasema.