http://www.swahilihub.com/image/view/-/3509904/thumbnail/1529424/-/lrwpgo/-/desa.jpg

 

Chonde chonde maliza mgomo wa madaktari, Mong'are aambia Uhuru

Kennedy Mong'are

Seneta wa Nyamira Kennedy Mong'are Okong'o ahutubia wanahabari katika hoteli ya Serena, Nairobi baada ya kutangaza kuingia ulingoni kuwania urais Desemba 27, 2016 

Na WANDERI KAMAU

Imepakiwa - Sunday, January 8  2017 at  12:48

Kwa Mukhtasari

Seneta Kennedy Mong’are wa Nyamira amemlaumu Rais Uhuru Kenyatta akidai anachangia Wakenya kuhangaika kwa kutotatua mgomo wa madaktari unaoendelea.

 

SENETA Kennedy Mong’are wa Nyamira amemlaumu Rais Uhuru Kenyatta akidai anachangia Wakenya kuhangaika kwa kutotatua mgomo wa madaktari unaoendelea.

Mbali na hayo, ametaja hali ya njaa katika baadhi ya sehemu nchini, hali ya ufisadi Serikalini, ukabila kati ya masuala mengine kama baadhi ya majukumu ambao rais amekosa kuyawajibikia.

Amesema kuwa rais anaonekana kutojali huku mamia ya Wakenya wakiendelea kufariki kutokana na mgomo wa madaktari.

“Ni dhahiri kwamba kutotatuliwa kwa mgomo huo kunawanyima Wakenya haki ya kuishi, kulingana na Kipengele 26 cha katiba, ambacho kinaihitaji Serikali kutoa huduma muhimu kama afya kwa kila Mkenya. Hii ni sawa na kuwaua, kinyume na kuyalinda maisha yao,” akasema Bw Mong’are.

Ameeleza kuwa kijumla, Rais Kenyatta amevunja vipengele 16 vya katiba, hilo likiwa kinyume na kiapo chake cha kuilinda na kuitetea.

Matatizo ya tangu uhuru

Vilevile amelaumu Serikali ya Jubilee kwa kukosa kushughulikia matatizo yaliyoikumba Kenya tangu uhuru, badala yake 'ikiyaongeza kupitia ukabila, viwango vya juu vya ufisadi na ukosefu wa ajira'.

“Ni wakati Wakenya wazinduke ili kuikomboa nchi yao. Uongozi wa sasa umefeli kabisa kutatua changamoto zinazowakumba,” akasema.

Seneta huyo pia alikosoa uzinduzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo na Serikali ya Jubilee kama Reli ya Kisasa (SGR), akisema haiwafaidi wananchi kwa vyovyote vile, ikizingatiwa kuwa baadhi ya maeneo inayopitia yanakumbwa na ukame.