http://www.swahilihub.com/image/view/-/3449858/medRes/436101/-/y4iyd3z/-/kalwiper.jpg

 

Chunga ulimi wako, Kalonzo amuonya Muthama

Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka

Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka akihutubu awali. Picha/MAKTABA 

Na STEPHEN MUTHINI

Imepakiwa - Wednesday, May 24  2017 at  12:17

Kwa Muhtasari

KIONGOZI wa Chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, amemtaka Seneta wa Machakos, Johnstone Muthama, akome kumdharau la sivyo asahau kabisa matumaini ya kumpigia debe mgombeaji urais wa muungano wa NASA, Raila Odinga.  

 

Akiongea katika Kanisa la AIC Kasina, Mlolongo, Bw Musyoka alisema kamwe hajamsaidia yeyote kupata ushindi popote nchini wakati wa mchujo wa chama cha Wiper, kinyume na madai ya Seneta Muthama.

Bw Musyoka alisisitiza kuwa Bw Muthama hawezi kumfanyia kampeni Bw Odinga bila kukipigia debe chama cha Wiper. “Ninamtaka Seneta Muthama akubaliana na uongozi wa chama kwa sasa. Yeye hawezi kusema mambo tofauti na msimamo wa chama,” akasema Kalonzo ambaye ni mgombea mwenza wa muungano wa NASA.

Alitaja msimamo wa Bw Muthama kuwa hatari kwa umoja wa NASA na kuonya kuwa huenda akachukua hatua inayoweza kutafsiriwa vibaya.

“Utafika wakati ambapo nitamtaka Bw Odinga kuweka wazi iwapo angependa kushirikiana kisiasa na Muthama au Kalonzo,” akaongeza.

Kauli ya Bw Musyoka inatokana na msimamo mkali wa Bw Muthama, unaoonyesha anaegemea upande wa Bw Odinga.
Hata wakati wa kumteua mgombeaji urais wa NASA, inasemekana kuwa Bw Muthama alikuwa mstari wa mbele kumpigia debe Bw Odinga, jambo lililomkera Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa, Bw Francis Nyenze.

Bw Muthama alitofautiana na uongozi wa chama cha Wiper baada ya Naibu Gavana wa Machakos Bernard Kiala kubwagwa na Bi Wavinya Ndeti kwenye mchujo wa Wiper.

Bw Muthama amekuwa akimuunga mkono Bw Kiala kutwaa tiketi ya Wiper kuwania ugavana wa Kaunti ya Machakos.

Kwa mtazamo wake, Bw Muthama, ambaye ametangaza kuwa hatagombea wadhifa wowote wa kisiasa, anamchukulia mgombeaji wa Wiper, Bi Wavinya Ndeti, kuwa mtu kutoka nje, ambaye alijiunga na chama hicho dakika za mwisho na akapewa nafasi ya kuwania.

Kufikia mwezi Aprili mwaka huu, Bi Ndeti alikuwa kiongozi wa Chama Cha Uzalendo (CCU).

Seneta huyo pia alikasirishwa na jinsi chama hicho kilisimamia mchujo wa ugavana Kitui ambapo Seneta David Musila alishindwa na Gavana Julius Malombe.

“Wakati mlisikia nikisema sitatetea kiti changu ni kwa sababu ya dhuluma za kisiasa alizoonyeshwa Seneta Musila,” akasema Bw Muthama wakati wa mazishi ya mama ya Bw Musila, Jumamosi iliyopita.

Alidai Gavana Malombe alitumia ukora kupata ushindi, madai ambayo Dkt Malombe alikanusha. “Waliosimamia mchujo huo wa Kitui waliandika barua yenye maelezo ya kuhusu wizi huo lakini hakukuchukuliwa hatua yoyote. Bw Malombe anafaa kuzuiwa kugombea,” akasema Bw Muthama.

Bw Muthama na Bw Kiala hawakuhudhuria mkutano wa chama cha Wiper mjini Machakos Ijumaa iliyopita kumpigia debe Bi Ndeti.

Mnamo Jumapili, Gavana wa Makueni, Kivutha Kibwana, Bi Ndeti, Mbunge wa Mavoko Patrick Makau, na mwenzake wa Matungulu, Stephen Mule, walihutubia wananchi eneo la Mlolongo lakini Bw Muthama hakuwepo.

Mwaka jana wakiwa kwenye ziara ya kisiasa kaunti ya Makueni, wawili hao walitofautiana, pale Bw Muthama alipomtaka gavana wa kaunti hiyo, Prof Kivutha Kibwana kuvunja chama chake na kujiunga na Wiper.

Ilimbidi Bw Muthama ajiondoe katika msafara na kurejea Nairobi.
Wakati huo Kalonzo alimlaumu Muthama kwa kuhujumu nafasi yake ya kuwa mgombea urais wa uliokuwa muungano wa Cord.