http://www.swahilihub.com/image/view/-/3468772/medRes/1479511/-/2hg78f/-/ngc.jpg

 

Cord Mlima Kenya yadai Uhuru anajifanya refarii 2017

Rais Uhuru Kenyatta

Rais Uhuru Kenyatta akihutubu awali. Picha/PSCU 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Saturday, January 7  2017 at  18:33

Kwa Mukhtasari

Mrengo wa Cord eneo la Mlima Kenya wamemtaka Rais Uhuru Kenyatta aelewe waziwazi kuwa hawezi akawa mwaniaji wa urais 2017 na pia awe ndiye refarii wa kuthibiti sheria za mchezo huo.

 

MRENGO wa Cord eneo la Mlima Kenya wamemtaka Rais Uhuru Kenyatta aelewe waziwazi kuwa hawezi akawa mwaniaji wa urais 2017 na pia awe ndiye refarii wa kuthibiti sheria za mchezo huo.

Umemtaka aelewe kuwa uchaguzi mkuu ni shughuli ya kitaifa ambayo umiliki wa hisa zake ni wa taifa lote na vyama vyote vinavyowania nyadhifa.

“Huwezi katika hali hiyo ukiwa ni mmoja tu wa wale watakaokuwa katika mchezo huo wa kutwaa ushindi uwe ndiye wa kutoa sheria za kufuatwa. Ni
hali ambayo itazua utata na itie doa shughuli yote ya uchaguzi huo. Kwa hilo, sioni ni kwa nini asiitishe mdahalo wa wadau ili waafikiane
kuhusu utata wa sheria za kufuatwa,” akasema Bw Wambugu Kioi, katibu wa muungano wa Cord kwa vijana wa eneo hilo.

Akiongea mjini Kerugoya, Bw Kioi alisema kuwa kuna haja kubwa kwa rais atulize hali ya utata inayokumba kupitishwa kwa mabadilioko ya
kisheria kuhusu uchaguzi 2017 ambapo mabunge yote mawili (la kitaifa na Seneti) yaliungana na kutumia idadi yao ya kuifaa serikali kupitisha sheria hizo.

“Hizi ni sheria za Jubilee, sio za Wakenya. Hakufai kuwa na taswishi kuhusu nia ya sheria hizo. Huu ni uchaguzi wa kila Mkenya na kila mwaniaji na kunafaa kuwa na uwiano wa kimaoni kuhusu utaratibu wa uchaguzi huo. Vinginevyo ni sawa na wizi wa kura hata kabla ya siku ya kura kuwadia,” akasema.

Alisema kuwa Rais anapotoshwa na wandani wake kuwa mrengo wa Cord unapendelea mfumo wa kidijitali kuendesha shughuli hiyo ili kutatiza
uhalali wa uchaguzi huo.

“Kile hawaonekani kuelewa ni kuwa mrengo wa Cord pia umewekeza katika hisa za uchaguzi wa 2017 na hauwezi kukubali kwenda hasara kupitia
kutatiza kuandaliwa kwa uchaguzi huo. Cord pia tunaelewa kuwa sio lazima tuwe katika uchaguzi huo kwa kuwa ni wa hiari lakini tuko na
ari ya kupata mamlaka ya kisiasa kwa njia halali iliyojaa uwazi wa haki,” akasema.

Kutakasa

Alisema kuwa ni juu ya Rais atakase uchaguzi huo wa 2017 kuwa amejituma kuhakikisha uadilifu umedhihirika na haegemei upande ambao
anajua utamfaa kivyake huku Wakenya wengine nje ya ufuasi wake wakidunishiwa haki zao za kushiriki mchakato wa uchaguzi mkuu.