http://www.swahilihub.com/image/view/-/2959302/medRes/1178183/-/stah63/-/DnEldUhuru1511c.jpg

 

DP chataka mgao wa bajeti ya kumpigia debe Uhuru

Uhuru Kenyatta na William Ruto

Rais Uhuru Kenyatta pamoja na Naibu wa Rais William Ruto, ahutubia wananchi mjini Eldoret kabla kufululiza kwa Ikulu ndogo Novemba 15, 2015. Picha/JARED NYATAYA 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Sunday, January 8  2017 at  15:07

Kwa Mukhtasari

Chama cha Democratic Party (DP) sasa kinakitaka chama cha Jubilee Party (JP) kitengee fedha vyama vyote vinavyompigia debe rais Uhuru Kenyatta achaguliwe tena 2017.

 

CHAMA cha Democratic Party (DP) sasa kinakitaka chama cha Jubilee Party (JP) kitengee fedha vyama vyote vinavyompigia debe rais Uhuru Kenyatta achaguliwe tena 2017.

Kimesema kuwa “kwa sasa ni wazi kuwa kuna hali ya dharura ya kuwarai wapiga kura walio katika ngome zetu wajitokeze kwa wingi kumpigia Rais Kenyatta kura la sivyo chombo chake kizamishwe na upinzani.”

Akiongea Jumamosi mjini Nyeri, mwenyekiti wa DP Bw Esau Kioni alisema kuwa “kwa kuwa sisi tumejitolea kusaidia Jubilee Party katika harakati
za kuwafurusha wapiga kura kutoka manyumbani mwao ili wakampigie kura rais, hatufai kubaguliwa na kutengwa kama maadui.”

Akasema: “Hiyo keki ya kufanya kampeni inafaa iwekelewe juu ya meza na yeyote anayewajibikia kampeni za rais akatiwe kipande. Sisi kama DP
tunagombea nyadhifa zinginezo kando na kile cha Urais. Kwa Rais tumesema ni Uhuru Tena lakini nyadhifa hizo zingine tumenyane kidemokrasia.”

Bw Kioni alisema kuwa mwelekeo wa 2017 utatolewa na jinsi wapiga kura watajitokeza kupiga kura.

“Ikiwa watu wetu hapa Mlima Kenya hawatajitokeza kwa zaidi ya asilimia 90 kumpigia kura Rais Kenyatta, pia wale ambao hawajajisajili wafanye
hivyo haraka iwezekanavyo na wamuunge rais mkono, basi tuko taabani. Ni vyema ieleweke kuwa vyama vidogo vilivyokaidi kujiunga na Jubilee
Party sio maadui bali ni watu wa mkono kumfaa rais,” akasema.

Alisema kuwa kwa sasa JP inasaidiwa Mlima Kenya na vyama vya Nark-Kenya, DP na PNU na kwa pamoja vyama hivyo havifai kubaguliwa bali vinafaa kujumuishwa katika mikakati ya kumpigia debe Rais.

Tiketi ya moja kwa moja

Alishikilia kuwa bado msimamo wa DP ni ule ule wa kuwapa wafuasi wake waaminifu tiketi ya moja kwa moja kuwania nyadhifa 2017.

“Hao ni wale wafuadi ambao wamekuwa wakitimiza matakwa yote ya chama tangu kizunduliwe mwaka wa 1991 na rais mstaafu Mwai Kibaki. Sisi
hatutawasumbua wawaniaji wetu kwa harakati nyingi kama mchujo. Anayetaka kuwania na ni mwanachama wetu mwaminifu atapata tiketi ya moja kwa moja bila kujali ushindani ambao atakuwa nao katika eneo lake la uwaniaji,” akasema.