DPP, EACC na wakili Omanga kushiriki kesi ya Maraga

Na RICHARD MUNGUTI

Imepakiwa - Wednesday, January 11  2017 at  16:31

Kwa Mukhtasari

MAHAKAMA kuu Jumatano ilimkubalia wakili Charles Omanga , mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP) Keriako Tobiko na tume ya kupambana na ufisadi (EACC) kushiriki katika kesi ambapo Jaji Mkuu (CJ) David Maraga ameshtakiwa kwa kutunga sheria za zitakazofuatwa na kitengo cha Mahakama kuu cha kuamua kesi za ufisadi.

 

Jaji Roselyn Aburili aliwakubalia Bw Omanga , Bw Tobiko, EACC na mamlaka ya kusaka mali iliyoibwa (ARA) kujiunga na kesi hiyo wamtetee Jaji Maraga.

“Vita ya kupigana na ufisadi itafaulu ikithibitiwa kutoka mahala pamoja ndipo wanaotweza haki wajulikane,” alisema wakili Samuel Adunda anayemwakilisha Bw Omanga.

Jaji Aburili aliamuru kesi hiyo isikizwe Januari 31,2017.

Jaji Maraga ameshtakiwa na wakili Peter Wanyama.

Kesi hiyo iliwasilishwa kwa mara ya kwanza Desemba 2016 mbele ya Jaji George Odunga alikataa kuisikiza akisema alikuwa mmoja wa majaji waliotunga sheria za kitengo hiki kipya cha kupambana na kesi za ufisadi.

“Sitatoa maagizo yoyote kuhusu kesi hii inayohusu kitengo nilichoshiriki kubuni sheria zake,” akasema Jaji Odunga na kuamuru “ Kesi hiyo isikizwe katika kitengo hicho kipya na Jaji Lydia Achode mnamo Janauri 11,2017.”

Jaji Odunga alisema kuwa kesi hiyo inazua masuala makubwa yenye umuhimu wa kitaifa kisha “kairatibisha kuwa ya dharura.”

Bw Adunda aliyewasilisha kesi hiyo alimweleza Jaji Odunga kwamba yeyote yule anayesaidia korti kuharakisha kuamuliwa kwa kesi za ufisadi zilizokaa mahakamani kwa miaka na mikaka anapasa kuungwa mkono.

“Ni wazi kwamba ufisadi umeisambaratisha nchi hii na kupelekea wengi kuangamia,” akasema Bw Adunda.

Alimsihi Jaji Odunga akubali kuratibisha kesi hiyo kuwa ya dharura.

Akitoa uamuzi Jaji Odunga alisema , “Sitatoa maagizo yoyote katika kesi hii kisa na maana nilikuwa mmoja wa majaji walioteuliwa kutunga sheria za idara hii mpya iliyozinduliwa rasmi na Jaji Maraga wiki mbili zilizopita.”

Jaji huyo alisema kuna kesi nyingine ambayo iliwasilishwa na Bw Wanyama akipinga sheria kwamba maombi yote ya kupinga mashtaka ya ufisadi kutoka kila pembe ya nchii yawe yakisikizwa katika kitengo hiki kipya.

Bw Wanyama anasema kuwa maagizo hayo ya CJ na sheria za kuthibiti idara hii mpya zinatwaa mamlaka ya majaji wale wengine wa Mahakama kuu katika kaunti ambao wanaweza kuamua maombi hayo.

Jaji Maraga alifichua akizindua idara hii kuna mahakimu 20 ambao wameteuliwa kusikiza na kuamua kesi za ufisadi.

Alisema kwa vile kitengo hiki kimebuniwa hivi punde kesi zote za kupinga mashtaka ya ufisadi yatakuwa yanasikizwa Nairobi.