http://www.swahilihub.com/image/view/-/2755780/medRes/1039250/-/b6xaasz/-/DNBungeVetting0906c.jpg

 

Kazi za kuvutia kule ughaibuni ni mtego, serikali yaonya

Monicah Juma

Bi Monicah Juma. Picha/BILLY MUTAI 

Na WANDERI KAMAU

Imepakiwa - Thursday, December 7  2017 at  18:52

Kwa Muhtasari

SERIKALI imewaonya Wakenya dhidi ya kuvutiwa na ahadi za kazi nzuri katika nchi za kigeni bila kufanya uchunguzi ufaao kuzihusu.

 

Katibu katika Wizara ya Mashauri ya Kigeni, Monicah Juma alisema Alhamisi kwamba, Wakenya wengi wameishia kutesekea katika nchi hizo, hasa wakati ahadi hizo zinageuka kuwa za uwongo.

Akiwakabidhi Wakenya wanne walioachiliwa nchini Sudan Kusini kwa familia zao jijini Nairobi, Dkt Juma aliwashauri kuhusisha wizara hiyo, ili kuwapa mwongozo ufaao kuepuka matatizo katika nchi hizo.

“Ni vizuri muwe mkichunguza kwa kina ahadi zinazotolewa na mashirika ya kimataifa kuhusu kazi za ughaibuni. Baadhi huwa mitego ya kuwaingiza katika masaibu yasiyoisha,” akaonya Dkt Juma.

Wanne hao ni Anthony Keya, Boniface Muriuki, Ravi Ghadhda na Anthony Mwadime.

Watu hao walikamatwa mjini Juba mnamo Mei 2015 pamoja na wengine 12, ambapo walipatikana na makosa ya njama za wizi.

Walikuwa wamehukumiwa kifungo cha maisha gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kupanga njama za kuiba Sh1.4 bilioni kutoka afisi ya Rais Salva Kiir.

Walizuiliwa kwa siku 40 bila kuhojiwa. Walikuwa wakifanya kazi katika kampuni ya Click Tecknologies.

Akihutubu kwa niaba yao, Ravi aliishukuru serikali na Wakenya kwa kuwaombea, na kuwawezesha kuachiliwa.

“Tunawashukuru nyote kwa juhudi za kutuwezesha kuachiliwa, na hatimaye kuungana na familia zetu,” akasema Ravi.

Rais Kenyatta alifanikiwa kuishinikiza Sudan Kusini kuwaachilia baada ya kufanya mkutano na Rais Kiir baada ya kuapishwa kwake. Duru zilisema kwamba mwafaka huo ulifikiwa baada ya mkutano huo.