http://www.swahilihub.com/image/view/-/3095876/medRes/1267463/-/y31d3r/-/CECILYKARIUKI.jpg

 

FIDA yamuomba Uhuru awape wanawake zaidi uwaziri

Bi Cecily Kariuki

Waziri wa Utumishi wa Umma, Vijana na Masuala ya Jinsia Bi Sicily Kariuki akihutubu awali. Picha/ HISANI 

Na WANDERI KAMAU

Imepakiwa - Wednesday, December 6  2017 at  19:09

Kwa Muhtasari

CHAMA cha Mawakili Wanawake nchini (FIDA) Jumatano kilimtaka Rais Uhuru Kenyatta kuwateua wanawake zaidi katika baraza la mawaziri.

 

Aidha, kinamtaka rais kuhakikisha kuwa wanawake wanajumuisha angaa thuluthi moja ya baraza hilo, kulingana na  Katiba.

Kwenye barua ya wazi kwa Bw Kenyatta Jumatano, mwenyekiti wake, Bi Josephine Wambua, alisema kuwa wako tayari kumwasilishia rais orodha ya wanawake wenye uwezo, kwa nafasi 22 za uwaziri anazotarajiwa kuzitangaza.

“Tunakuomba kuhakikisha kwamba umewateua angaa wanawake saba katika baraza lako, kwani litawapa nafasi zaidi wanawake, kwani wametengwa kwa muda mrefu, hasa kwenye utaratibu wa uongozi wa nchi,” akasema Bi Wambua.

Baraza la sasa lina mawaziri watano, wakiwemo; Bi Amina Mohamed (Wizara ya Mashauri ya Kigeni), Phyllis Kandie (Leba), Reychelle Omamo (Ulinzi) na Sicily Kariuki (Jinsia na Masuala ya Vijana) na Prof Judi Wakhungu (Mazingira).

Aliyekuwa Waziri wa Ugatuzi Anne Waiguru, ambaye sasa ni gavana wa Kirinyaga, aliondoka barazani baada ya kukabiliwa na tuhuma za ufisadi katika Huduma ya Kitaifa kwa Vijana (NYS) ambapo zaidi ya Sh791 milioni zinakisiwa kupotea.

Rais Kenyatta anatarajiwa kulitangaza baraza lake wiki ijayo, baada ya kukutana na uongozi wa Bunge la Kitaifa, ili kuwawezesha wabunge kuwapiga msasa wale watakaoteuliwa.

Na kinyume na sasa, ambapo baraza hilo linawajumuisha mawaziri 18, duru zinasema kuwa rais analenga kuliongeza hadi mawaziri 22, huku akiwashirikisha wanasiasa zaidi, kuliko ilivyo sasa.

Kulingana na kipengele 27 (8) cha katiba asasi zote za umma zinahitajika kuhakikisha kuwa zinajumuisha angaa thuluthi moja wa wafanyakazi wake kuwa wanawake.

Hata hivyo, uzingatiaji wa sheria hiyo ungali kibarua, hasa baada ya Bunge kukosa kupitisha sheria hiyo. Lakini katika kujitetea kwao, FIDA ilimwomba rais kutimiza ahadi ya kuwashirikisha wanawake zaidi katika utawala wake.

“Tunakuomba kutimiza ahadi yako, kwani hilo litakuhakikishia uungwaji mkono zaidi kutoka kwa wanawake,” akasema.

Mashirika mbalimbali yamekuwa yakijitokeza kuwarai Rais Kenyatta na Naibu Rais William Ruto kuyakumbuka katika uteuzi huo.