http://www.swahilihub.com/image/view/-/2729718/medRes/975784/-/dfbpp3z/-/DNBungePAC1803t.jpg

 

FKE yampapura Aden Duale

Aden Duale

Kiongozi wa Wengi Bungeni Aden Duale akihutubu awali. Picha/BILLY MUTAI 

Na CHARLES WASONGA

Imepakiwa - Tuesday, February 13  2018 at  12:17

Kwa Mukhtasari

Afisa Mkuu Mtendaji wa Shirikisho la Waajiri Nchini (FKE) Jaqueline Mugo amepuuzilia mbali kauli ya kiongozi wa wengi bungeni Aden Duale kwamba amedumu katika bodi ya Hazina ya Malipo ya Uzeeni (NSSF) kwa muda mrefu kinyume na sheria.

 

AFISA Mkuu Mtendaji wa Shirikisho la Waajiri Nchini (FKE) Jaqueline Mugo amepuuzilia mbali kauli ya kiongozi wa wengi bungeni Aden Duale kwamba amedumu katika bodi ya Hazina ya Malipo ya Uzeeni (NSSF) kwa muda mrefu kinyume na sheria.

Afisa huyo amefafanua kuwa anahudumu kipindi cha kwanza katika bodi hiyo baada ya kuteuliwa kwa kipindi cha miaka mitatu chini ya sheria mpya ya NSSF ya 2013, na kwamba suala hilo lilikwisha kuamuliwa na mahakama.

Kwenye taarifa iliyochapishwa magazetini Jumanne Bi Mugo anasema uteuzi wake ulifanywa pamoja na ule wa Katibu Mkuu wa Muungano wa Wafanyakazi (Cotu) Francis Atwoli.

“Uteuzi huo ulifanywa na aliyekuwa kaimu Waziri wa Leba Raychelle Omamo mnamo Septemba 16, 2015, kupitia ilani iliyochapishwa kwenye gazeti rasmi la serikali toleo nambari 6752. Hii ina maana kuwa mimi na Bw Atwoli tunahudumu muhula wetu wa kwanza kama wanachama wa Bodi ya Wadhamini wa NSSF," Bi Mugo ameeleza.

Wiki jana Mbunge huyo wa Garissa Mjini alimtaka Waziri Mteule wa Leba wa Ukur Yatani awaondoe Bi Mugo na Katibu Mkuu wa Muungano wa Wafanyakazi Nchini (Cotu) Francis Atwoli kama wanachama wa Bodi ya NSSF endapo ataidhinishwa katika wadhifa huo.

Mugo na Atwoli wanawakilisha waajiri na wafanyakazi mtawalia, katika bodi hiyo.

“Wawili hao wamedumu kwa zaidi ya miaka sita katika bodo hiyo kinyume cha Sheria ya sasa," akasema Bw Duale.

Ahadi

Naye Bw Yatani aliahidi kutekeleza pendekezo hilo akisema hiyo ndiyo itakuwa kazi yake ya kwanza atakapoingia afisini ikiwa bunge litaidhinisha Jumanne kuteuliwa kwake.

Jumatatu, Mugo alitaja kauli ya Duale kama ambayo ilitolewa bila uelewa wa sheria na uzingativu wa uamuzi wa mahakama ya Leba ambayo ilimaliza mvutano uliokuwepo kuhusu suala hilo kabla ya sheria hiyo mpya kuanza kutumika.

Wiki jana Bw Atwoli alikuwa wa kwanza kumrukia Bw Duale kwa kutoa pendekezo hilo alilodai ni la kupotosha na kutilia shaka uhalali wa nafasi yake, na Bi Mugo, katika bodi hiyo.

Bi Mugo alionya maafisa wa serikali na wanasiasa dhidi ya kuingilia shughuli za bodi ya NSSF akiahidi kutekeleza wajibu wake katika bodi hiyo kwa ushirikiano na wanachama wengine.