http://www.swahilihub.com/image/view/-/4843712/medRes/2164972/-/i5vssu/-/visaluni.jpg

 

Gathoni Wa Muchomba awapiga jeki vijana kujiendeleza kibiashara

Gathoni Wa Muchomba

Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Kiambu katika Bunge la Kitaifa Bi Gathoni Wa Muchomba akitoa vifaa vya ususi na vinyozi kwa vijana wanaoendesha biashara zao mjini Thika Novemba 8, 2018. Picha/LAWRENCE ONGARO 

Na LAWRENCE ONGARO

Imepakiwa - Friday, November 9  2018 at  10:36

Kwa Muhtasari

Wasusi na vinyozi wanufaika kwa kupata vifaa kazi chini ya mpango wa Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Kiambu katika Bunge la Kitaifa Bi Gathoni Wa Muchomba uliopewa jina la 'Mamacare'.

 

THIKA, Kenya

VIKUNDI vya vijana 269 walioungana chini ya mwavuli wa Thika Barbers and Salon Association, vimepokea vifaa kazi kutoka kwa Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Kiambu katika Bunge la Kitaifa Bi Gathoni Wa Muchomba.

Bi Wa Muchomba, alisema mradi huo wa kuwainua vijana kuendesha biashara zao ni wa takribani Sh1.5 milioni.

"Ni muhimu kuinua vijana waweze kuendesha biashara bila kunyanyaswa katika mazingira salama. Nitazidi kuwasaidia vijana, walemavu, na hata wanawake bila kurudi nyuma," alisema Bi Wa Muchomba akihutubu Alhamisi mjini Thika wakati akiwapa vijana vifaa ikiwemo vile vya ususi na ulimbwende kwa jumla.

Alimkosoa Gavana wa Kiambu Bw Ferdinand Waititu kwa kuongeza ushuru ambao wafanyabiashara wa chini wanatozwa; jambo alilosema linastahili kupingwa.

Alimshauri Bw Waititu kusikiza sauti ya mwananchi kwa sababu akiendelea kuongeza ushuru, bila shaka mwananchi wa chini atafinyika pakubwa.

Alisema vijana 200 watajiunga na vyuo vya kiufundi ili kujifunza kozi tofauti zitakazowafaidi katika siku za usoni.

"Watu wanaotamani kurejea darasani watapewa nafasi kuhudhuria masomo ya jioni. Wale walio tayari wajiandikishe mara moja," alisema Bi Wa Muchomba.

Alisema kwa wakati huu viongozi wote wanastaahili kuelekeza akili zao katika ajenda nne zilizopendekezwa na Rais Uhuru Kenyatta kwa muda wa miaka minne ijayo.

Pesa hazitoshi

Mwakilishi huyo alisema fedha anazopokea kutoka kwa hazina ya serikali ni Sh4 milioni pekee na ambazo haziwezi kutosheleza mahitaji ya kaunti ndogo 12 katika kaunti nzima ya Kiambu.

"Fedha hizo kutoka kwa hazina ya serikali ni kiwango kidogo mno. Ingekuwa bora kiasi kikaongezwa na kufikia angalau Sh25 milioni ili ziweze kutosheleza mahitaji yaliyo muhimu ya kubadilisha maisha ya wananchi tunaowawakilisha," alisema Bi Wa Muchomba.

Alisema kwa muda wa mwaka mmoja sasa, amewapeleka walemavu 500 shuleni.

Alisema vijana wanaobeba mizigo kwa mabega na makuli kwenye masoko na stesheni watanufaika kutoka kwake lakini ikiwa tu watafuata masharti kadha.

Alisema atawanunulia kijigari cha kusukuma aina ya toroli ambacho kitakuwa kikiwasaidia kubebea wanunuzi na wateja wengine mizigo yao.

"Niko tayari kuwasaidia vijana watakaoacha uraibu wa pombe haramu. Ningetaka pia kijana kama huyo awe na mchumba ili aweze kuwa na majukumu ya kifamilia," alisema Bi Wa Muchomba.

Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Elgeyo Marakwet, Bi Jane Chebaibai alisema eneo lake lina kaunti ndogo nne na ameweza kusaidia vikundi 10 vya akina mama ili kujiendendeleza.

Chebaibai alitoa mwito kwa viongozi wengine kuzingatia maendeleo badala ya siasa za pesa nane.

"Mimi katika eneo langu ninafanya bidii kwa kuona ya kwamba watu ninaowakilisha wananufaika kutokana na miradi tofauti ya maendeleo," alisema Bi Chebaibai.