Wakazi wa Gatuanyaga wasema barabara ni mbovu katika eneo lao

Na LAWRENCE ONGARO

Imepakiwa - Friday, February 1  2019 at  10:55

Kwa Muhtasari

Wakazi wa Gatuanyaga wanasema barabara huwa hazipitiki wakati wa mvua na kukiwa na kiangazi vumbi linakuwa ni tele.

 

THIKA, Kenya

WAKAZI wa Gatuanyaga na vitongoji vyake Thika Mashariki, wanateta kuhusu hali mbaya ya barabara.

Wakazi hao wanasema ya kwamba wakati wa mvua magari ya uchukuzi hasa matatu hukosa kufika mashinani, huku wakati wa kiangazi vumbi pia likiwa ni tele.

Wakazi hao wanataka kaunti ya Kiambu kujitokeza wazi na kufanya jambo ili hali ya usafiri iweze kuimarika.

"Sisi wakazi wa eneo hili tunataka serikali ya kaunti ya Kiambu izinduke na kuziba mashimo mengi yanayoshuhudiwa barabarani katika eneo hili," alisema Peter Kimani ambaye ni mkazi wa Gatuanyaga.

Watu walioathirika pakubwa ni wasafirishaji mawe ya ujenzi kwa malori.

Walilalama pia kwamba watozaji ushuru huwa katika mstari wa kwanza kusanya pesa za ada ya ushuru, huku wakidai miguu ya malori hayo hupasuka kila mara.

Wahudumu wa bodaboda nao hawakuachwa nyuma kulalamika huku wakisema wanasafiri mwendo wa kilomita 15; eneo zima la barabara likiwa na mashimo mengi.

Hata hivyo, mnamo Alhamisi mbunge wa Thika Bw Patrick 'Wa Jungle' Wainaina, alizindua mradi wa ukarabati barabara ya Gatuanyaga-Munyu-Githima ambapo ilitandazwa murram ili kupunguza shimo tele zilizoko kwenye barabara hiyo.

Kuelezea kero

"Nyinyi ambao ni wapigakura mna nafasi ya kuelezea kero yenu ili mfanyiwe kazi na viongozi wenu," alisema Bw Wainaina.

Wakazi hao walisema iwapo kaunti ya Kiambu haitachukua jukumu la kufanya marekebisho, nao hawatakubali kulipa ushuru wanaotozwa kila mara.

Walisema viongozi wengi kama diwani, seneta na mbunge mwakilishi wa kike kutoka kaunti ya Kiambu, baada ya kuchaguliwa wao hupotea wasionekane kabisa.

Bw Wainaina alisema Wakfu wa Jungle utaendelea kuwahudumia watu wake.

Alisema tingatinga linalokarabati barabara za mashinani hutumia kiasi kikubwa cha hela.

"Kwa muda mchache ambao tingatinga hilo limefanya ukarabati eneo la Gatuanyaga na vitongoji vyake gharama imekuwa ni Sh500,000.

Aliwahimiza wakazi hao wawe wakiwahimiza viongozi hapo kuwaletea maendeleo na hilo ni jukumu lao.

"Nyinyi kama wapigakura mna haki kamili ya kufanyiwa kazi kwa sababu ni haki yenu," alisema Bw Wainaina.