Kembi Gitura akemea madai ya Wetang'ula ya ufisadi seneti

Seneta wa Murang'a Kembi Gitura

Seneta wa Murang'a Kembi Gitura wakati wa mahojiano mjini Murang'a Januari 26, 2015. Picha/JOSEPH KANYI 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Wednesday, January 11  2017 at  17:44

Kwa Mukhtasari

Naibu spika wa Seneti Bw Kembi Gitura ametaja madai ya Seneta wa Bungoma Bw Moses Wetang’ula kuwa serikali kuu iliiba kura za kupitisha sheria tata za uchaguzi wa 2017 kama ya 'kitoto'.

 

NAIBU spika wa Seneti Bw Kembi Gitura ametaja madai ya Seneta wa Bungoma Bw Moses Wetang’ula kuwa serikali kuu iliiba kura za kupitisha sheria tata za uchaguzi wa 2017 kama ya 'kitoto'.

Amesema kuwa ni aidha Bw Wetang’ula amepoteza uhalisia wa maadili anayohitajika kutilia mkazo kama kiongozi, au “kwa mpigo mmoja ameanza
kuishiwa na ulainifu mawazoni.”

Bw Gitura aliye pia Seneta wa Murang’a alisema kuwa “nimemsikiza Wetang’ula akiwa katika mkutano huo wao wa Bomas akisema kuwa serikali
iliiba kura za kupitisha sheria hizo katika Seneti.”

Alisema kuwa yeye kama Wakili sawa na Bw Wetang’ula, alishindwa kuelewa “hata ikiwa ni siasa tunacheza bora tusiwe na adabu kiasi za kusema yasiyoweza kukuletea balaa baadaye.”

Alisema kuwa madai ya Wetang’ula kuwa “kuna madalali wa serikali kuu waliokuwa wakizu9nguka katika bunge la Seneti wakiwahonga maseneta
ili wapige kura ya kupitisha sheria hizo ni madai mazito sana yanayomwangazia kama aliye na habari muhimu kuhusu ukora wa kimaadili.”

Alisema kuwa matamshi yake yalimwangazia kama aliye na nia hata ya kuchoma bunge la seneti kwa njia ya kuipotezea sifa na sura kwa umma.

“Angewataja waliokuwa naye wakihongwa. Ikiwa ni wale waliopiga kura za kuunga mkono sheria hizo, rekodi za Seneti ziko wazi na ziliwanakili.
Ni juu ya Bw Wetang’ula ajitoe kimasomaso na kutwambia ni nani aliyehongwa ili kupiga kura,” akasema Gitura mjini Murang’a.

Ukumbini

Aliteta kuwa yeye akiwa mmoja wa waliokuwa ukumbini mwa Seneti, “sikushuhudia yeyote akihongwa na nimeshtuka sana kumwona Wetang’ula ambaye alikuwa katika bunge hilo akipambana kufa kupona kuangusha kura hizo akisema kuwa pia alikuwa akishuhudia hongo ikitanda Seneti.”

Alisema kuwa uongozi wa Wetang’ula umejaliwa utundu wa kila aina na amejumuika miongoni mwa wale ambao hawawezi kukubali sio lazima maoni
yao yawe ndiyo yanakubalika na wengi.

“Akishindwa, ameibwa ushindi. Wasiomuunga mkono, wamenunuliwa. Wasiomujumuisha serikalini, ni wezi… Huo sio ulainifu wa kimawazo kamwe,” akasema.