http://www.swahilihub.com/image/view/-/4195122/medRes/1815070/-/11c8xv8z/-/OU.jpg

 

Hofu na machafuko baada ya uamuzi wa mahakama

Lori

Lori hili liliteketezwa na waandamanaji wenye ghadhabu katika mtaa wa Migosi, mjini Kisumu Novemba 20, 2017 baada ya Mahakama ya Juu kuamua kuwa Rais Kenyatta alishinda uchaguzi wa Oktoba 26 kihalali. PICHA/ RUSHDIE OUDIA  

Na  Rushdie Oudia, Barack Oduor, Elisha Otieno, Joel Reyia, Benson Amadala, Derick Luvega na Vivere Nandiemo

Imepakiwa - Monday, November 20  2017 at  15:44

Kwa Muhtasari

WANANCHI katika maeneo mengi ya Nyanza na Magharibi mwa Kenya Jumatatu waliendelea na shughuli zao za kawaida baada ya Mahakama ya Juu kutoa uamuzi wake kuhusu matokeo ya uchaguzi wa marudio wa urais.

 

Fujo zilishuhudiwa katika Kaunti ya Kisumu na Migori ambapo barabara kadhaa zilifungwa na waandamanaji.

Vijana wenye ghadhabu walichoma gari na kuwasha moto barabarani Kisumu huku wakikagua kila gari lililopita.

Walishambulia watu watatu waliokuwa kwenye gari dogo wakawapiga na kuwapora kabla kuchoma gari hilo. Watu hao walitorokea kituo cha polisi cha Kondele. Mbali na mitaa ya Kibuye na Kondele, hali ilikuwa tulivu katikati mwa mji huo.

Katika Kaunti ya Migori, waandamanaji waliziba barabara kuu ya kuelekea Isebania. Hata hivyo, maeneo mengi ya kaunti hiyo yalikuwa tulivu na wakazi waliohojiwa wakasema wanasubiri wapewe mwelekeo na Kinara wa NASA, Bw Raila Odinga.

Wafanyabiashara Homa Bay waliamua kufunga maduka yao kwa kuhofia maandamano yenye ghasia lakini kulikuwa na utulivu.

Wafuasi wengi wa Muungano wa NASA walisema wanasubiri kinara wa muungano huo, Bw Raila Odinga, awaambie hatua atakayochukua.

“Mahakama ya Juu imekosea kwa kukubali uchaguzi wenye ulaghai,” akasema Bw Walter Opiyo, mkazi wa eneo hilo.

Utulivu ulishuhudiwa pia katika Kaunti ya Vihiga ambapo wafanyabiashara waliendelea na shughuli zao za kawaida.

Mbunge wa Sabatia, Bw Alfred Agoi, alikuwa ametoa wito wa utulivu kabla Mahakama ya Juu itoe uamuzi wake.

“Tuna mpango wetu wa kurudisha hadhi ya nchi. Tunataka kurudisha haki ya uchaguzi,” akasema.

Viongozi wa NASA katika Kaunti ya Narok walisema uamuzi uliotolewa hauna maana kwa sababu Wakenya wengi hawakushiriki katika uchaguzi huo.

“Kutokana na kuwa wanachama wa NASA na idadi kubwa ya Wakenya hawakushiriki kwenye uchaguzi, uamuzi uliotolewa hauna maana na unamaanisha matakwa ya watu wachache ndiyo yanapewa kipaumbele,” akasema seneta wa kaunti hiyo, Bw Ledama ole Kina.

Kulikuwa na utulivu pia Kakamega ambapo wakazi waliendeleza shughuli zao za kawaida.

Hata hivyo, wakazi kadhaa wa Mumias Mashariki ambako ni ngome ya kisiasa ya Jubilee katika kaunti hiyo walijitokeza kusherehekea uamuzi wa mahakama.

Hali tulivu ilishuhudiwa pia katika Kaunti ya Siaya ingawa wakazi walikosoa Mahakama ya Juu kwa kukubali ushindi wa Rais Kenyatta licha ya makosa mengi yaliyotokea wakati wa uchaguzi wa marudio wa Oktoba 26.

Mkazi wa eneo hilo, Bw James Okombo, alimtaka Bw Odinga achukue hatua haraka ili Jubilee izuiliwe kutawala kwa njia zisizofaa.

“Tunahofu kuhusu hatua zitakazochukuliwa na rais. Kuna uwezekano atavuruga ugatuzi na Bunge la Wananchi. Raila anafaa atupe mwelekeo,” akasema Bw Okombo.