Huduma ya Mastercard kuwafaa wenye vioski

Na BERNARDINE MUTANU

Imepakiwa - Wednesday, December 6  2017 at  19:16

Kwa Muhtasari

HUDUMA ya Mastercard Jumatano ilizindua jukwaa la kidijitali kwa wafanyibiashara wadogo kuwa na uwezo wa kuagiza bidhaa kielektroniki.

 

Huduma hiyo ilizindua Kionect, kwa lengo la kuwasaidia wamiliki wa vioski Nairobi kuagiza bidhaa kwa wingi na kulipa wauzaji wa bidhaa hizo kwa kutumia simu.

Kupitia kwa jukwaa hilo, watakuwa na uwezo wa kupata mikopo pamoja na kupata orodha ya bidhaa walizonunua kwa njia rahisi.

Mradi huo imezinduliwa kwanza katika mitaa ya mabanda ya Kibera, Kawangware na Kariobangi ambapo wamiliki 1,000 watahusishwa.

Huduma hiyo itatolewa kwa kushirikiana na mfanyibiashara wa kuuza bidhaa kwa jumla Kaskazi, na Benki ya Diamond Trust ambayo itarahisisha shughuli ya kulipia bidhaa kwa mfumo wa dijitali.

Ili kupata mikopo, mkopeshaji (Musoni) atakagua orodha ya shughuli katika mfumo wa Kionect wa kila mfanyibiashara anayetaka ufadhili wa fedha.

Kila mmoja atakuwa na uwezo wa kupata fedha zaidi kwa kulipa mkopo kwa wakati ufaao.