http://www.swahilihub.com/image/view/-/4958260/medRes/1940454/-/13060b/-/nkatha.jpg

 

IEBC: Chebukati alaumiwa na aliyekuwa naibu wake

Consolata Nkatha-Maina

Consolata Nkatha-Maina ambaye alikuwa Naibu Mwenyekiti wa IEBC akajiuzulu Jumatatu, Aprili 16, 2018. Picha/MAKTABA  

Na CHARLES WASONGA

Imepakiwa - Wednesday, January 30  2019 at  13:12

Kwa Muhtasari

Ufichuzi huo unajiri huku Kamati ya Bunge kuhusu Uhasibu (PAC) ikiuliza jinsi IEBC ilivyotoa zabuni ya thamani ya Sh700 milioni kwa kampuni mbili za teknolojia kutoa huduma wakati wa uchaguzi mkuu wa 2017.

 

NAIROBI, Kenya

ALIYEKUWA naibu mwenyekiti wa Tume huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Consolata Maina Jumanne alimkashifu Mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati kwa kuamuru kuamuru ukaguzi wa idara ya teknolojia ya habari na mawasiliano (ICT) bila kuwafahamisha makamishna wenzake.

Ufichuzi huo ulijiri huku Kamati ya Bunge kuhusu Uhasibu (PAC) ikiuliza jinsi IEBC ilivyotoa zabuni ya thamani ya Sh700 milioni kwa kampuni mbili za teknolojia kutoa huduma wakati wa uchaguzi mkuu wa 2017.

Alipofika mbele ya kamati hiyo Bi Maina aliwaambia wabunge wanachama kwamba Bw Chebukati aliwasilisha ripoti hiyo katika kamati ya makamishna wote na kusisitiza kuwa mjadala kuihusu iwe sehemu ya ajenda.

Alisema makamishna hawakuwa na habari kwamba mwenyekiti huyo alikuwa ameagiza ukaguzi ufanye.

“Mwenyekiti aliondoa ripoti kutoka mvunguni mwa meza na akatuletea,” Bi Maina akasema.

Huku akisema Bw Chebukati ndiye alikuwa chimbuko la mgawanyiko miongoni mwa makamishna na maafisa wa kuu wa tume hiyo kuelekea uchaguzi mkuu wa 2017, Bi Maina alikana madai kuwa makamishna waliamuru uagizaji wa bidhaa wa moja kwa moja..

“Kazi ya utoaji tenda ilikuwa ni ya afisi kuu chini ya usimamizo wa Afisa Mkuu Mtendaji. Kazi yetu ilikuwa ni kutoa ushauri pekee kuhusu masuala ya sera na taratibu,” akasema.

Kupitisha zabuni

Bi Maina alielezea wabunge wanachama wa PAC jinsi Bw Chebukati alivyowalazimisha makamishna kupitisha zabuni kadha badala ya kujenga mwafaka, akiongeza kuwa walipoingia afisini nyingi za zabuni zilikuwa zimekwisha kukamilishwa.

“Sikuhusishwa katika utoaji zabuni yoyote. Kila kitu kilifanyika katika kiwango cha kamati ya makamishna wote,” akawaambia wanachama wa PAC.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo Opiyo Wandayi alikosoa jinsi IEBC iliharikisha utoaji zabuni mbalimbali katika kipindi cha wiki mmoja baaada ya kandarasi husika kutiwa saini.

Wabunge, wakiwemo Junet Mohammed (Suna Mashariki) na Tom Kajwang (Ruaraka) walitaka kujua jisni kampuni za IBM East Africa na Oracle Technology Systems Kenya zilishindania zabuni katika IEBC.

Kulingana na zabuni hizo, IBM ilipaswa kutoa huduma za mitambo, usalama wa programu mbalimbali na ushauri, kati ya huduma nyinginezo kwa bei ya Sh483 milioni.

Kwa upande wake huduma ya Oracle Database and Security Solutions ilinunuliwa kwa bei ya Sh273 milioni.