NCCK: IEBC ipewe nafasi itekeleze majukumu yake

Peter Karanja

Katibu Mkuu wa Baraza la Makanisa Nchini (NCCK) Mchungaji Peter Karanja kwenye kongamano la siku tatu lililofanyika ukumbi wa Jumuia Kainti ya Kilifi. Picha/WACHIRA MWANGI  

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Wednesday, August 9  2017 at  13:54

Kwa Mukhtasari

Muungano wa makanisa nchini (NCCK) umewataka wanasiasa na wananchi kuipa tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC mwanya wa kuendesha majukumu yake kikamilifu kufuatia uchaguzi mkuu uliofanyika mnamo Jumanne Agosti 8 kote nchini.

 

NAIROBI, Kenya

MUUNGANO wa makanisa nchini (NCCK) umewataka wanasiasa na wananchi kuipa tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC mwanya wa kuendesha majukumu yake kikamilifu kufuatia uchaguzi mkuu uliofanyika mnamo Jumanne Agosti 8 kote nchini.

"Ninaomba Wakenya wadumishe amani huku tukisubiri shughuli ya uhesabu wa kura ikamilike na tujue mshindi ni nani. Turejee kwenye kazi zetu na tuepuke matamshi yanayochochea ghasia," amesema katibu mkuu wa NCCK Kasisi Peter Karanja akihutubia waandishi wa habari Jumatano jijini Nairobi.

Amefichua kuwa NCCK imefanya mkutano wa faragha na IEBC na tume hii imesema inafanya majukumu yake kama ilivyoahidi taifa kupitia mwenyekiti wake Bw Wafula Chebukati.

"Tumefaenya mkutano na IEBC muda mfupi uliopita, wamesema watatekeleza wajibu wao kama walivyoahidi," akaeleza akiongeza kwamba tume hiyo imeahidi kuonyesha fomu 34A ambayo imezua utata kwa Nasa.

Nasa na Jubilee kukutana

NCCK aidha imeshauri mrengo wa Jubilee na muungano wa upinzani, National Super Alliance (Nasa), kufanya mkutano ili kujadili umuhimu wa amani nchini.

"Wakenya wadumishe amani, matokeo ya kura yakitangazwa kuwepo na ambaye hataridhishwa nayo atumie njia inayofaa kueleza tetesi zake ili tusirejeshe taifa kwa visa kama vilivyotokea mwaka wa 2007/2008," akasema Kasisi Karanja.

Ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka wa 2007 zilipelekea takriban watu 1,300 kuuawa na maelfu kufurushwa kutoka makwao.

"Nasa na Jubilee ni Wakenya wenzetu, tudumishe amani," akaongeza.

NCCK aidha imepongeza IEBC kwa utendakazi wake. "Wameonyesha ukakamavu kwa kuendesha uchaguzi kwa mpangilio mwema na wenye amani tele," akasema Bw Karanja.

Muungano wa Nasa aidha unapinga matokeo ya kiti cha urais yanayoendelea kuhesabiwa, kujumuishwa na kupeperushwa na IEBC ukihoji hayana uhalisia.