IMF yamteua Mkenya kukagua matumizi ya fedha

Na BERNARDINE MUTANU

Imepakiwa - Wednesday, December 6  2017 at  19:21

Kwa Muhtasari

Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF) limemteua Mkenya, Dkt Nancy Asiko Onyango kuwa mkurugenzi wake katika afisi ya kuchunguza matumizi ya fedha na ukaguzi (OIA).

 

Meneja Mkurugenzi wa IMF Christine Lagarde Jumanne alisema Dkt Asiko ana uzoefu wa miaka 25 katika ukaguzi wa hesabu za fedha, na utaalam huo unaifaa sana IMF.

Dkt Asiko pia ni mtaalam katika masuala ya kudhibiti hali hatari, usimamizi wa mashirika na tishio la mfumo wa habari na mawasiliano.

“Zaidi ya uzoefu wake katika usimamizi wa mashirika, Nancy anapenda sana kuwakuza wanawake na wasichana hasa katika masuala ya uongozi. Ni mshauri nasaha wa wasichana kutoka familia maskini ulimwenguni,” alisema Lagarde alipotangaza uteuzi wake.

Dkt Asiko ataanza kazi Februari 2018 kuchukua mahali pa Clare Brady aliyeondoka IMF.

Kabla ya kuteuliwa, alikuwa Mkurugenzi Mkuu katika Shirika la Reliance Risk Advisory Solutions, Kenya na alikuwa mshirikishi PwC Kenya kwa wakati mmoja.