http://www.swahilihub.com/image/view/-/3096768/medRes/597198/-/khmlxh/-/DNLENKU2809B.jpg

 

Jamvi: Ulimbukeni wa kisiasa wa mawaziri ulivyomtoa jasho Uhuru

Joseph ole Lenku

Aliyekuwa waziri wa Usalama Joseph ole Lenku. Picha/ANN KAMONI 

Na WANDERI KAMAU

Imepakiwa - Thursday, November 9  2017 at  17:36

Kwa Muhtasari

UKOSEFU wa utetezi wa kisiasa wa serikali kutoka baraza la sasa la mawaziri, umedaiwa kumfanya Rais Uhuru Kenyatta kutathmini kuwateua wanasiasa zaidi kama mawaziri.

 

Duru zinasema kuwa, ingawa Bw Kenyatta anangoja uamuzi wa Mahakama ya Juu kupitisha ama kufutilia mbali kuchaguliwa kwake kama rais mnamo Oktoba 26, huenda akawatema mawaziri wengi.

Mbali na hayo, imeibuka kwamba Bw Kenyatta anapanga kuongeza nafasi za mawaziri kutoka 19 hadi 22, kama mkakati wa kuipanua serikali yake.

Ripoti zinasema kwamba hatua ya rais imechangiwa pakubwa na kimya cha mawaziri wengi, hata anapokumbwa na changamoto za kisiasa, hali ambayo imemfanya kujipata pabaya kila anapokosolewa na wapinzani wake.

Wachanganuzi wa masuala ya kisiasa wanasema kwamba ni lazima Bw Kenyatta awateue mawaziri wengi wanasiasa, kwani amelazimika kujitetea binafsi, mawaziri wengi wakionekana kuwa kivuli tu.

Funzo

“Bw Kenyatta amejipata pagumu sana katika kipindi chake cha kwanza, hali ambayo inapaswa kuwa funzo kwa kiongozi yeyote atakayewania urais kuzingatia makini sana kuwateua mawaziri ambao wana tajriba fulani ya kisiasa,” asema Godfrey Sitati, ambaye ni mchanganuzi wa masuala ya kiutaeala.

Kulingana Bw Sitati, mawaziri wengi walisahau kwamba kando na kutekeleza majukumu yao ya kitaaluma, wana majukumu ya kisiasa, hasa kuitetea serikali.

Asema kuwa kutokana kimya hicho, imewalazimu Bw Kenyatta na naibu wake William Ruto kuzidisha majukumu yao kuwatetea mawaziri, kwani wengi wao walikuwa wataalamu, wasio tajriba yoyote ya kisiasa.

Mifano inayotolewa ni aliyekuwa Waziri wa Ugatuzi Bi Anne Waiguru, ambaye alilazimika kujiuzulu kutokana na ukosoaji mkubwa wa kinara wa NASA Raila Odinga na washirika wake kutokana na sakata ya ufisadi katika Huduma ya Kitaifa ya Vijana (NYS). Bw Odinga ndiye alifichua sakata hiyo ambapo zaidi ya Sh791 milioni zinadaiwa kupotea.

Ole Lenku

Mfano mwingine ni aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Joseph Ole Lenku, ambaye alilazimika kujiuzulu kutokana na ukosoaji mkubwa baada ya kushindwa kuhimili mawimbi ya Upinzani, kuhusu alivyoiendesha wizara hiyo.

Mchanganuzi Felix Kavii asema kwamba licha ya kuwa walikosa kuwajibika kwa namna moja ama nyingine, ukosefu wa tajiriba na ujasiri wa kisiasa kuujibu Upinzani ndiyo uliowafanya kujiuzulu.

“Katika suala la Bi Waiguru, Rais Kenyatta alijaribu kwa namna yoyote kumtetea, ila alishindwa. Ikiwa Bi Waiguru angekuwa na uzoefu wa kisiasa, angeweza kuwakabili wakosoaji wake kwa njia huru, bila msaada wowote kutoka kwa rais,” asema Bw Kavii.

Hilo linalinganishwa na serikali za awali, ambapo mawaziri waliwajibu wapinzani wao bila kuogopa lolote, hivyo kutompa rais wakati mgumu kuitetea serikali.

Mfano ni aliyekuwa Waziri wa Fedha Amos Kimunya, aliyesema “heri afe badala ya kujiuzulu” mnamo 2008, baada ya kuhusishwa na sakata tata ya uuzaji Hoteli ya Laico Regency, wakati huo ikiwa Grand Regency.

“Kwa ujasiri kama huo, Rais Mstaafu Mwai Kibaki hakuwa na ugumu wowote, kwani mawaziri waliwakabili wakosoaji wao wenyewe bila mwingilio wa rais,” asema Bw Kavii.

Kuokoa hali

Wachanganuzi wanasema kuwa udhaifu huo ndio ulimfanya Rais Kenyatta kuwateua mabw Mwangi Kiunjuri (kama Waziri wa Ugatuzi) na Eugene Wamalwa (kama Waziri wa Maji) kwani alijipata akiwatetea mawaziri ambao kimsingi walipaswa kujitetea wenyewe.

 Kulingana na Prof Macharia Munene, ambaye ni mchanganuzi wa kisiasa, mawaziri wanapaswa kuwa na ujasiri wa kisiasa, licha ya kuwa wanataaluma.

Asema kuwa udhaifu wa katiba ya sasa ni kutotambua kwamba kinyume na mataifa yenye demokrasia pevu kama Amerika na Uingereza, Kenya ingali demokrasia changa inayodhibitiwa pakubwa na mielekeo ya kisiasa.

“Muundo wa katiba ya sasa ulilenga kuwapa mawaziri nafasi ya kutekeleza majukumu yao pasi mwingilio wowote wa kisiasa. Hata hivyo, hilo lilikuwa kosa, kwani waundaji wake walikosa kutambua kwamba wangali wanategemewa kutekeleza majukumu ya kisiasa, kwa mfano kuitetea serikali dhidi ya ukosoaji wa Upinzani,” asema Prof Munene.

Ujasiri wa Matiang'i

Mchanganuzi huyo anamtaja Waziri wa Elimu Fred Matiang’i kama mfano bora wa mwanataaluma aliyefahamu  majukumu yake ya kisiasa na kuyatekeleza vizuri. Asema kwamba ujasiri wa  Dkt Matiang’i ndio umemfanya kukosolewa pakubwa na wanasiasa.

Mbali na hayo, amsema kwamba hilo ndilo lilimfanya Rais Kenyatta kumteua kama Kaimu Waziri wa Usalama wa Kitaifa.

“Kile mawaziri wengi walikosa kufahamu ni kwamba kinyume na mazingira ya kitaaluma walimokuwa, kazi ya serikali ni ya kisiasa. Hilo ndilo limewafanya baadhi yao kutoonekana au kutosikika kabisa katika wizara wanazosimamia,” asema Bw Prof Munene.

Wachanganuzi wanasema kuwa ombwe hilo linapaswa kuwa funzo kuu kwa kiongozi yeyote anayechaguliwa rais katika siku za usoni, kuzingatia tajriba ya kisiasa, kwani itamfaa, hasa kuhimili ukosoaji wa Upinzani.