http://www.swahilihub.com/image/view/-/4801358/medRes/2137600/-/13ivs81/-/kocha.jpg

 

Jinsi kocha Ochieng alivyokomboa maisha ya vijana Githurai

Kocha wa All Stars Githurai, Fredrick Ochieng akiwa na vijana ambao anawanoa vipaji vyao. Picha/ SAMMY WAWERU  

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Thursday, October 11  2018 at  14:50

Kwa Muhtasari

Wazo la kuanzisha timu hii lilinijia baada ya kuona vijana wamepotelea kwa uhalifu

 

Nairobi. Fredick Ochieng ndiye kocha na mwanzilishi wa timu ya All Stars inayowakilisha mtaa tajika wa Githurai, Nairobi na Kiambu katika soka.

Historia ya mtaa huu ikinakiliwa, jina la Ochieng halitakosa kujumuishwa. Awali, Githurai ilifahamika kudorora kwa usalama, visa vya uhalifu vikiwa sajili ya kila siku katika vituo vya polisi. “Ungezuru mitaa mingine ufichue umetoka Githurai, watu wangekuepuka wakikuhusisha na uhalifu,” Ochieng alieleza kwenye majojiano maalum na Swahili Hub.

Licha ya wasifu huo, mtaa huu sasa umekuwa uga wa kuwekeza katika sekta ya biashara. Ochieng ni mmoja wa wazalendo waliosaidia kuimarisha hali ya usalama.

Mwaka 1998 visa vya vijana kuuawa kwa sababu ya kujihusisha na uhalifu vilimshawishi kocha huyu kukomboa mta huo kwa kuanzisha timu ya soka, ‘All Stars Githurai’ ambayo kwa sasa imekuwa kigezo cha mabadiliko.

“Wazo la kubuni timu hii lilinijia baada ya kuona vijana wamepotelea kwa uhalifu. Wazo hilo sasa ndilo limekuwa daraja la vijana kupata ajira, na kujiepusha na uhalifu,” alisimulia Ochieng.

“Wanasoka Amos Nodi, Francis Kahata wanaochezea Gor Mahia, Dunstan Kugo, Calvin Otieno na Simon Mbugua wa Rangers, pamoja na Peter Nzuki wa Tusker, wote wamepitia mikononi mwangu katika timu ya All Stars Githurai,” alisema.

Ingawa kukabiliana na uhalifu ilikuwa sawa na kukwea Mlima Everest kwa kutumia kandambili, kocha Ochieng alisema asingestahimili kuona nafsi za vijana ambao ndio viongozi wa kesho zikiangamia.

Pili, yeye kama mzazi alikuwa na jukumu kuona vijana wanakua kwa uadilifu na zaidi ya yote kunoa vipaji vya chipukizi. “Kuna vipaji vingi sana vya soka, voliboli, riadha, michezo ya kuigiza, na sanaa,” alieleza.

Ni kupitia juhudi za Ochieng ambapo mtaa wa Githurai umeonekana kuwa na taswira mpya. Minghairi ya ufanisi aliopata, safari yake haijakosa changamoto za hapa na pale, na alisema ukosefu wa fedha za kutosha ndio kizingiti kikuu cha kunoa vipaji katika kabumbu. “Upungufu wa jezi, viatu na uga maalum wa kufanyia mazoezi na hata kuandaa mechi ndizo changamoto zinazonikabili,” alifichua. Ufadhili wa timu hiyo hutegemea wasamaria wema, na baadhi ya viongozi na mashirika yanayojitolea kuwapa msaada.

Timu hiyo ni ya wachezaji walio na umri kati ya miaka 17-30, na iliyoweza kunoa vipaji wanaochezea timu za kitaifa nchini.

Kwa sasa inashiriki mechi za ligi ya Super 8, 2018 inayojumuisha timu 16 za mitaa mbalimbali kaunti ya Nairobi kama Makadara JLSA, Jericho All Stars, Shaurimoyo All Stars, Kawangware United, Derpotivo Rongai, na Kayole Asubuhi.

Ochieng alisema ana imani kuwa timu yake itachukua kombe la Super 8, 2018. “All Stars Githurai ingali kifua mbele mechi zote tulizoshiriki. Tuna matumaini makuu tutashinda tuzo ya mwaka huu ya Sh500, 000,” alisema. Mwaka uliopita, timu hii iliibuka kidedea kwenye tonamenti ya ligi hiyo na kupokea Sh100, 000.

Kocha huyu alisema shabaha yake ni kuona nyota alionao katika All Stars Githurai wakikwea kiwango cha kucharaza ngoma ya ligi ya kitaifa, KPL, na ile ya kimataifa ya Uingereza, EPL.