Jirongo taabani zaidi, atakiwa kumlipa Atwoli Sh110 milioni

Na  RICHARD MUNGUTI

Imepakiwa - Thursday, October 12  2017 at  20:14

Kwa Mukhtasari

MWANIAJI kiti cha urais katika uchaguzi mkuu wa Agosti 8,2017 na mbunge wa zamani wa Lugari Cyrus Jirongo alijipata taabani zaidi Alhamisi Mahakama kuu ilipomwamuru amlipe katibu mkuu wa muungano wa vyama vya wafanyakazi (SG) Francis Atwoli zaidi ya Sh110milioni.

 

Agizo hili lafuatia amri ya kumtangaza Bw Jirongo amefilisika aliposhindwa kulipa deni la Sh110milioni.

Jaji Francis Tuiyot alisema katika uamuzi aliotoa Alhamisi kwamba Bw Jirongo anapasa kumlipa Bw Atwoli alizomkopesha. 

Katika ushahidi aliowasilisha kortini , Bw Jirongo aliitikia kwamba alipokea Sh100 milioni kutoka kwa Bw Atwoli na atamlipa kwa riba ya Sh10milioni.         

Bw Jirongo, aliyepata umaarufu wakati wa vuguvugu la Youth for KANU almaarufu YK-92 alikuwa amemuahidi SG wa COTU kwamba atamlipa akipokea malipo kutoka kwa baraza la jiji la Nairobi.

Alikuwa ameiuzia baraza hili NCC ardhi kupitia kwa kampuni yake Kuza Farms and Allirf Limited.

Alikuwa amemsihi Bw Atwoli asubiri apokee malipo hayo kutoka kwa NCC.

Jaji Francis Tuiyot alitupilia mbali ushahidi wa Bw Jirongo na kusema “anatakiwa kumlipa Bw Atwoli Sh110milioni.”