K.U mbioni kuzalisha megawati 10 za umeme kutokana na jua

Na BERNARDINE MUTANU

Imepakiwa - Wednesday, December 6  2017 at  19:04

Kwa Muhtasari

CHUO Kikuu cha Kenyatta kimezindua awamu yake ya mwanzo ya mradi wa umeme kwa kutumia jua.

 

Chuo hicho kilizindua awamu hiyo Jumanne. Mradi huo unaogharimu Sh1.7 bilioni unalenga kukifanya chuo hicho kuwa na uwezo wa kujitengenezea umeme, kwa lengo la kupunguza gharama ya umeme kutoka mfumo wa umeme wa kitaifa.

Mradi huo ulizinduliwa katika bewa kuu, Thika Road, ambapo awamu hiyo ina uwezo wa kutoka kilowati 100. Iligharimu Sh17 milioni kufanikisha awamu hiyo.

Mradi wote unalenga kutoa megawati 10. Umeme utakaozalishwa katika awamu ya pili utauziwa serikali, kwa lengo la chuo hicho kuimarisha mapato yake.

Awamu ya mwanzo ilisakiniwa na shirika la Ufaransa la Urbasolar kupitia kwa ufadhili wa serikali ya Ufaransa, na umechukua ekari tatu za ardhi ya chuo hicho.

Serikali imekuwa ikitekeleza mpango wa kuimarisha viwango vya uzalishaji wa umeme kwa kulenga njia zingine za kupata umeme ikiwemo ni pamoja na matumizi ya upepo na gesi.

Mradi huo ulizinduliwa na Waziri wa Kawi Bw Charles Keter.