Wakfu wa KCB kufadhili wanafunzi 240 elimu ya sekondari

Na BERNARDINE MUTANU

Imepakiwa - Wednesday, December 6  2017 at  15:26

Kwa Muhtasari

Wanafunzi 240 waliofanya vyema katika mtihani wa darasa la nane watapewa ufadhili wa elimu na Wakfu wa KCB mwaka ujao.

 

Wakfu huo umefungua nafasi ya kutuma maombi ya ufadhili huo kwa mwaka wa 2018, ambapo wanafunzi watakaofaulu watapata ufadhili wa masomo yao kwa miaka minne.

Wanafunzi hao watahitajika kusomea katika shule za umma chini ya mpango huo.

Kati ya nafasi 240 zilizotolewa, nafasi 40 zimetolewa kwa wanafunzi walio na changamoto za kimaumbile, vipofu na viziwi.

“Lengo la ufadhili huo ni kuwapa elimu bora wanafunzi werevu na maskini na wale walio na ulemavu kwa kuwapa ufadhili wa masomo na ushauri,” alisema Mkurugenzi Mkuu wa Wakfu wa KCB Jane Mwangi wakati wa uzinduzi wa programu hiyo Jumatatu, Nairobi.

Wakati wa kutuma maombi ni hadi Desemba 14, 2017 ambapo mahojiano yatafanywa kote nchini kati ya Desemba 15 na 16, alisema.

Watakaozingatiwa ni waliofanya vyema zaidi katika KCPE mwaka huu katika kiwango cha kaunti, na waliosomea katika shule za msingi za umma.

Pia, lazima wathibitishe wanahitaji ufadhili huo, na lazima wawe wameitwa katika shule ya sekondari ya kitaifa, kaunti au shule za hadhi ya juu katika kiwango cha kaunti.

Ufadhili huo utagharamia karo, sare na vitabu, na wanafunzi hao watapata mshauri kutoka tawi lao la Wakfu wa KCB.