KEBS kutwaa magari 110 yasiyolipiwa kodi

Na BERNARDINE MUTANU

Imepakiwa - Wednesday, December 6  2017 at  14:56

Kwa Muhtasari

Shirika la Kudhibiti Ubora wa Bidhaa (KEBS) huenda likatwaa magari 110 baada ya wamiliki wake kushindwa kulipia magari yao kodi kwa wakati ufaao.

 

Magari hayo yalitengenezwa 2010 na wamiliki wake wana hadi Desemba 31 kulipa kodi hiyo, au magari hayo yatwaliwe na kurudishwa yalikonunuliwa.

Kodi hiyo huwa lazima kwa kila gari linaloingia nchini kutoka soko la kimataifa miaka minane baada ya kutengenezwa.

Meneja Mkurugenzi wa KEBS Bw Charles Ongwae alisema ingawa Shirika la Kutoza Ushuru (KRA) limewapa wamiliki wa magari hadi Januari 17 kukamilisha kulipia ada magari yao, nafasi hiyo ya wiki mbili haitanufaisha wamiliki wa magari yaliyoundwa 2010 kwa sababu yatakuwa na zaidi ya miaka nane.

Serikali imezuia ununuzi wa magari yaliyoundwa zaidi ya miaka nane iliyopita kwa sababu hayafai. Badala ya kuyaruhusu kuingia nchini, serikali huyarudisha tena kwa mataifa yalikotoka.

KEBS ilisema inashirikiana na KRA ili kuhakikisha kuwa magari hayo hayachukuliwi baada ya muda huo kukamilika kwa kukataa kuyasajili.

“Yeyote aliyenunua gari lililotengenezwa 2010 anafaa kumalizana nasi kabla ya Desemba 31,” alisema Bw Ongwae.

Wiki tatu zilizopita, KRA ilitoa ilani kwa wamiliki wa magari 163 walioshindwa kulipia ada bandarini, kwamba magari hayo yatapigwa mnanda ikiwa wamiliki wake hawatamaliza kuyalipia kabla ya Januari 17.