KQ yazimwa kuwatimua wafanyakazi

Na BERNARDINE MUTANU

Imepakiwa - Wednesday, December 6  2017 at  19:07

Kwa Muhtasari

SHIRIKA la Ndege la Kenya Airways limesimamishwa na mahakama kuwafuta kazi wafanyikazi wa kifundi waliogoma wiki iliyopitwa.

 

KQ ilisamishwa na mahakama Jumanne kuwafuta kazi wahudumu wake 130 walioshtumiwa kwa madai ya kuhusika katika mgomo haramu.

Shirika hilo haliwezi kuwafuta kazi mpaka kesi iliyowasilishwa mahakamani na wafanyikazi hao kusikilizwa na kuamuliwa.

Shirika hilo liliwaandikia barua za kuwafuta kazi wahudumu hao na kutangaza nafasi zao katika magazeti ya humu nchini Ijumaa, Desemba 1. Wahudumu hao walikuwa pamoja na mafundi wa ndege.

Agizo hilo lilitolewa na jaji wa Mahakama ya Leba Hellen Wasilwa chini ya ombi la dharura lililowasilishwa na wahudumu hao kupitia kwa wakili wa Bw Dismas Wambola.

Kulingana na wafanyikazi hao, KQ haikuwapa nafasi ya kujitetea kabla ya kuwapa barua za kuwafuta kazi.

Bw Wambola alieleza mahakama kuwa mgomo wao haukuwa haramu kama ilivyodai KQ. Kesi hiyo itasikilizwa Desemba 18.