http://www.swahilihub.com/image/view/-/3208204/medRes/1320120/-/he4c2d/-/DNEradCo.jpg

 

KWAHERI 2016: Watu na matukio yaliyozua mijadala

Jacob Juma

Marehemu Jacob Juma. Picha/MAKTABA 

Na LEONARD ONYANGO

Imepakiwa - Sunday, January 1  2017 at  15:07

Kwa Mukhtasari

MWAKA wa 2016 ulijawa na mbwembwe pamoja na matukio mbalimbali yaliyogonga vichwa vya habari. Yafuatao ni miongoni mwa matukio na watu waliozua mjadala mkali nchini:

 

1. Dkt Fred Matiang’i
Waziri wa Elimu Dkt Matiang’i aligonga vichwa vya habari kutokana na utendakazi wake bora katika sekta ya elimu.

Mbali na kukabiliana na tatizo sugu la wizi wa mitihani ya kitaifa ya Darasa la Nane (KCPE) na Kidato cha Nne (KCSE).

Kadhalika, Dkt Matiang’i ameweza kusafisha sekta ya elimu licha ya kuhamishiwa katika wizara hiyo katika kipindi cha chini ya miaka miwili.

2. Maandamano
Muungano wa Cord uliongoza maandamano kila Jumatatu kati ya Mei na Juni kushininiza makamishna wa Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuondoka afisini.

3. Jacob Juma
Alikuwa mfanyabiashara na mkosoaji mkubwa wa serikali. Aliuawa kinyama na watu wasiojulikana jijini Nairobi.

Juma alimshambulia mara kwa mara Naibu wa Rais William Ruto kuhusiana na madai ya kuhusika na ufisadi kupitia akaunti yake ya Twitter.

Alitabiri kifo chake mwenyewe kuwa angeuawa.

4. Miguna Miguna
Mwaniaji wa ugavana wa Kaunti ya Nairobi aliwaaibisha wapinzani wake wa kike Margaret Wanjiru na Esther Passaris katika runinga.

Miguna ambaye huzungumza kwa majivuno alisababisha kutamatishwa kwa kipindi cha Jeff Koinange Live Show katika runinga ya KTN kwa kutoa matamshi ya kudhalilisha wanawake.

5. Boniface Mwangi
Aligonga vichwa vya habari aliposhtakiwa na Naibu wa Rais William Ruto kwa kumharibia jina kupitia mtandao wa Twitter.

Alishangaza Wakenya alipofichua kuwa alifanya mtihani wa KCSE mwaka jana akiwa na umri wa miaka 33.

6. Josephine Kabura Irungu
Msusi aliyegeuka kuwa milionea. Aliacha Wakenya vinywa wazi alipofichua kuwa kampuni zake zote 20 zilipata kandarasi katika wizara ya Ugatuzi bila kulipa ushuru.

Aliwashtua Wakenya zaidi aliposema kuwa alibeba zaidi ya Sh100 milioni katika magunia kwenda kulipa wahudumu wa timbo la mawe bila maafisa wa usalama.

7. Raila Odinga
Aliwakosesha viongozi wa serikali ya Jubilee usingizi kwa kufichua sakata moja baada ya nyingine.

Miongoni mwa sakata alizofichua ni madai ya kutoweka kwa fedha za mkopo wa Eurobond. Aliongoza maandamano ya kuondoa makamishna wa IEBC.

8. Jemimah Sumgong
Alijipatia nishani ya dhahabu mara mbili ndani ya mwaka mmoja. Alishinda dhahabu katika mashindano ya London Marathon na kisha katika mashindano ya Olimpiki yaliyofanyika mjini Rio de Janeiro, Brazil.

9. Rais Uhuru Kenyatta
Aligonga vichwa vya habari alipokiri katika Ikulu ya Nairobi kuwa ameinua mikono kwa kushindwa kukabiliana na ufisadi.

Kadhalika, alizua mjadala mkali alipoambia viongozi wa upinzani 'kuendelea kumeza mate huku wenzao wa Jubilee wakila nyama’ katika mazishi ya aliyekuwa mwanasiasa mkongwe William Ole Ntimama.