http://www.swahilihub.com/image/view/-/4185830/medRes/1808785/-/yh2302z/-/gaha.jpg

 

Mutahi Kahiga asema yeye daima atasalia kuwa mnyenyekevu

Mutahi Kahiga

Gavana Mutahi Kahiga wa Nyeri ala kiapo cha kuingia rasmi ofisini Novemba 13, 2017. Picha/JOSEPH KANYI 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Tuesday, November 14  2017 at  06:16

Kwa Muhtasari

Gavana mpya wa Nyeri, Mutahi Kahiga baada ya kulishwa kiapo cha huduma alisema kuwa wizi wa rasilimali za umma ni kama laana na hata kwa Mungu ni dhambi na kwamba ikiwa utashuhudia wizi wa rasilimali ukitekelezwa na uwe hutoi sauti yako kupinga, basi hata kwa Mungu utaulizwa uwajibikie kosa hilo la usaliti kwa kaunti yako.

 

SASA ni rasmi kuwa taifa hili lina magavana 47 kinyume na hali ya mpaka saa 10 Jumatatu ambapo kulikuwa na magavana 46.

Hii ni baada ya Naibu gavana wa Nyeri, Mutahi Kahiga, kuapishwa kutwaa majukumu ya gavana kamili katika Kaunti hiyo baada ya kifo cha Dkt Patrick Wahome Gakuru ambaye aliaga dunia katika ajali mbaya ya barabarani mnamo Novemba 7 katika Kaunti ya Murang’a.

Kuapishwa kwa Kahiga kumezua msisimko katika Kaunti hiyo kwa kuwa hotuba yake ya kukubali kutwaa majukumu hayo alijitaja kuwa binadamu wa kawaida ambaye hatabadilika katika "kuhusiana nanyi kwa msingi eti nimepanda ngazi".

Hotuba hiyo iliyotolewa kwa ufasaha mkuu wa lugha na mbwembwe za kujiangazia kama kiongozi shupavu asiye wa kupenda mzaha kazini alitilia mkazo kuboreka kwa maisha ya watu wa Nyeri, hasa alipotangaza kuwa hajaingia afisini kuvuruga msingi wa miezi mitatu ya utawala wa marehemu Gakuru.

Alisema kuwa baraza la mawaziri aliloteua marehemu Gakuru ndilo ataendelea mbele nalo na mengine mapya ni yale tu yatazuka lakini sio yale yatachangiwa na yeye kuvuruga msingi uliowekwa tayari.

“Mimi ni yule yule Kahiga ambaye mnamjua kama mwalimu na mtu wa kawaida mtaani na ambaye hatakoma kutangamana nanyi katika makanisa, barabarani, kwa baa, sokoni na kila mahali ambapo mwananchi wa Nyeri anaishi, hutafutia riziki, huabudia au kustarehe. Mimi sibadiliki kamwe,” akasema Kahiga.

Alisema yeye ni kiongozi hustler na ambaye hatachelea kuwa afisini na mitaani kuonekana na kila yeyote aliye na la kumwambia.

“Hasa wanyonge wetu wa Nyeri ambao shida yao kubwa ni kusombwa na mawazo ya kuelimisha watoto wenu…Ninyi ambao shida yenu ni kufanya biashara bila kusumbuliwa… Ninyi ambao shida yenu ni kusaka kazi… Tutashirikiana na mnihesabu kama kiungo muhimu katika kuklaa nanyi chini tukisaka afueni,” akasema.

Wizi wa raslimali

Kahiga aliahidi kupambana na wizi wa rasilimali za umma.

"Hakuna kitu nitachukulia kwa uzito kuliko yeyote atakayenaswa akijaribu kupora rasilimali za kuwapa watu wetu huduma,” akasema.

Kahiga alisema kuwa wizi ni kama laana na hata kwa Mungu ni dhambi.

"Ikiwa utashuhudia wizi wa rasilimali ukitekelezwa na uwe hutoi sauti yako kupinga, basi hata kwa Mungu utaulizwa uwajibikie kosa hilo la usaliti kwa kaunti yako,” akasema.

Kahiga ambaye alijitokeza kwa sura kamili ya mtetezi wa haki, ambapo alikuwa Katibu Mkuu wa Muungano wa Walimu (KNUT) eneo la Nyeri kabla ya kuteuliwa kuwa mgombezi mwenza na Dkt Gakuru alisema kuwa mwelekeo wake ni ule wa ushirika na wote wa wadau Nyeri, uvumilivu wa kimawazo kwa wakosoaji wake na pia kutetea ya haki kutendeka kwa jumuia ya watu wa Nyeri.

Alisema kuwa atategemea Mungu kumpa mwongozo na akipata ushirikiano wa dhati kutoka kwa wote walio uongozini wa kila ina eneo la Nyeri na pia wadau wote wakijumuisha raia wa kawaida, basi Nyeri itapaa juu kwa hadhi ya maendeleo.

Alisema kuwa atashirikiana kwa dhati na serikali ya Rais Uhuru kenyatta kuafikia manifesto ya utawala wa Jubilee “kwa kuwa sisi hapa Nyeri ni Jubilee kufa kupona na mwongozo wetu kisiasa ni Rais Kenyatta."