http://www.swahilihub.com/image/view/-/3449858/medRes/436101/-/y4iyd3z/-/kalwiper.jpg

 

Kalonzo amejiondoa mbio za kuingia Ikulu?

Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka

Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka akihutubu awali. Picha/MAKTABA 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Wednesday, January 11  2017 at  16:27

Kwa Mukhtasari

Kinara wa Wiper Bw Stephen Kalonzo Musyoka ameonekana kujikanganya kiusemi katika mkutano wa upinzani ukumbini Bomas kwa kutangaza kuwa yuko tayari kutupilia azma yake ya kuwania urais ndani ya muungano wa upinzani wa National Super Alliance (NASA).

 

KINARA wa Wiper Bw Stephen Kalonzo Musyoka alionekana kujikanganya kiusemi katika mkutano wa upinzani ukumbini Bomas Jumatano alipotangaza kuwa yuko tayari kutupilia azma yake ya kuwania urais ndani ya muungano wa upinzani wa National Super Alliance (NASA).

Umati uliokuwa umejitokeza kufuatilia mkutano huo na kuwasikiza viongozi wao haukumpa nafasi ya kurekebisha utelezi huo wa ulimi na aliishia kuangaziwa kama aliye nje ya kinyang’anyiro cha urais kwa tiketi ya upinzani.

“Mimi naweza nikatangaza hapa: Niko tayari kutupilia mbali azma yangu ya kuwa mgombea…” akasema kabla ya kukatizwa na shangwe na nderemo za
wawaniaji viti mbalimbali wa upinzani waliokuwa katika ukumbi huo.

Bw Kalonzo alitatizika pakubwa kuendelea kutoa ufafanuzi wake wa kile alichokuwa akimaanisha baada ya sherehe hizo za “kujitoa kwake” kinyang’nayironi kuendelea kumkatiza akiongea.

Ilikuwa wazi kuwa kilichomkanganya Bw Kalonzo ni ufasaha wa mpangilio wake wa lugha kwa kuwa ilikuwa dhahiri ujumbe wake mkuu ulikuwa 'sote
kama vinara wa vyama mbalimbali katika upinzani tunafaa kuondoa ubinafsi na tumuunge mkono yule atakayeteuliwa kwa njia ya haki na kweli kuwa mgombea wetu'.

Hata hivyo, Kalonzo aliendelea kutangaza vita dhidi ya serikali ya Jubilee akisema kuwa yeye mwenyewe amejitolea kutekeleza lote la uwezo wake kuuhakikishia mrengo wa upinzani ushindi katika uchaguzi mkuu wa 2017.

'Utawala mbaya'

Kalonzo alisema kuwa utawala wa Jubilee hauna mfano kote ulimwenguni kwa kuwa nki utawala ulio katika sifa za kipekee za “kuangamiza ndoto ya malengo pana ya Wakenya wote kwa jumla kuafikia afueni ya kimaisha.”

Alisema kuwa kujisajili kwa wapiga kura katika ufuasi wa upinzani ndio nguzo thabiti ya kutwaa ushindi.

Bw Kalonzo alidai kuwa kuna njama ambazo zimezinduliwa na serikali ya Jubilee za kutumia vitisho, hila na ujambazi katika kujinyakulia ushindi.

"Tunataka kuwaambia kuwa safari hii tumejitolea kuhakikisha kuwa tumefanya na kutekeleza lolote lililoko katika uwezo wetu kuchukua serikali baada ya uchaguzi wa Agosti 8, 2017,” akasema.