http://www.swahilihub.com/image/view/-/2355106/medRes/768998/-/5jfl5m/-/MainaKamanda.jpg

 

Maina Kamanda alaumiwa kupotezea JP umaarufu Nairobi

Maina Kamanda

Mbunge wa Starehe Maina Kamanda akiongea katika kikao cha awali na wanahabari Nairobi, Julai 24, 2013. Picha/ANTHONY OMUYA 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Sunday, January 8  2017 at  13:52

Kwa Mukhtasari

Wawaniaji wa nyadhifa kwa tiketi ya chama cha Jubilee Party eneo la Nairobi wamemtaka mbunge wa Starehe Bw Maina Kamanda akome kutoa matamshi ya kiholela kuhusu uchaguzi wa 2017.

 

WAWANIAJI wa nyadhifa kwa tiketi ya chama cha Jubilee Party eneo la Nairobi wamemtaka mbunge wa Starehe Bw Maina Kamanda akome kutoa matamshi ya kiholela kuhusu uchaguzi wa 2017.

Wameteta kuwa Bw Kamanda huwa na mazoea ya kupayuka kuhusu misimamo yake ya kibinafsi na kuifanya ichukuliwe kama msimamo wa chama cha Jubilee Party.

Mwenyekiti wa muungano huo Bw Samuel Maina akiongea na mtandao wa Swahilihub mjini Murang’a aliteta kuwa Bw Kamanda huwa na mazoea ya kujichukulia kama kinara wa JP Nairobi.

Aliteta kuwa shida kuu ya Bw Kamanda ni kukosa kuelewa athari za matamshi kiholela na uzinduzi wa miradi ya kisiasa isiyoambatana kamwe na mwelekeo wa makao makuu ya chama.

Bw Maina alisema kuwa Bw Kamanda iwapo hatathibitiwa, anaelekea kuzamisha uwezo kamili wa JP katika Kaunti ya Nairobi kama alivyofanya mwaka wa 2007 akiwa na chama cha PNU.

“Huyu Kamanda alianza kuweka vibarakala wake katika kila eneobunge la Nairobi katika uchaguzi mkuu wa 2007 ili kumenyana na wale waliokuwa wametambuliwa kuwa maarufu na wapiga kura. Aliishia kuzigawa kura za Nairobi kiasi kwamba PNU iliibuka na kura nyingi kwa Rais Mwai Kibaki lakini akiwa na upungufu mkubwa wa wabunge ambapo kila mwaniaji wa ODM alikuwa akipita kwa kura chache,” akasema.

Kamanda kubwagwa

Alisema kuwa hata yeye Bw Kamanda alijipata amezama katika njama zake ambapo alitimuliwa mamlakani kama mbunge wa Starehe na Askofu Margaret Wanjiru na hata baada ya kuwasilisha kesi mahakamani na akafanikiwa kujaribu tena kwenye uchaguzi mdogo, bado alishindwa na Bi Wanjiru.

“Sasa Bw Kamanda ako katika harakati za kumuunda mbunge wa Dagoretti Kusini Bw Dennis Waweru kuwa gavana wa Nairobi. Ametangaza kuwa hata
amesaka wapiga kura kutoka kaunti jirani ili wajisajili katika Kaunti ya Nairobi kumfaa Bw Waweru. Badala ya afanye hivyo na akae kimya, anatangaza hadharani kana kwamba wapinzani wetu ni viziwi,” akateta.

Aliteta kuwa Bw Kamanda haelewi kuwa Nairobi sio miliki ya jamii ya Agikuyu “na anafaa aelewe waziwazi na tena mchana hadharani kuwa hakuma Mugikuyu kwa sasa hivi anayeweza kutwaa ugavana wa Kaunti ya Nairobi ikizingatiwa 'ujumuiya' wa kura za makabila yaliyoko."

Bw Maina aliteta kuwa kwa saa hii, Bw Kamanda anaonekana akiunda wafuasi wake katika vikundi vya makabiliano “eti kutetea wafanyabiashara Nairobi iwapo mrengo wa Cord utazindua maandamano ya kupinga sheria tata za uchaguzi kama zilivyopitishwa na wabunge na maseneta.”

Akasema: “Mtu kama Kamanda anaturejesha katika utawala wa kujilinda badala ya kuwapa waliowajibishwa kutekeleza jukumu hilo kihalali kuwajibika. Bw Kamanda akiendelea katika mkondo wake wa sasa kisiasa, anatuelekeza katika shimo la giza Nairobi.”