http://www.swahilihub.com/image/view/-/4928530/medRes/2219930/-/f05p0oz/-/ra.jpg

 

Karlo yaahidi mbegu mpya za mahindi kukabiliana na fall armyworm

Fall armyworm

Fall armyworm ni hatari kwa mazao. Picha/MTANDAO 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Thursday, January 10  2019 at  08:23

Kwa Muhtasari

Fall armyworm ni hatari kwa mazao.

 

SHIRIKA la Utafiti na uimarishai teknolojia za mimea na mifugo nchini Kenya (Karlo) limeahidi wakulima wa mahindi kuwa litazindua mbegu mpya zenye uwezo wa kupambana na fall armyworm.

Katika kipindi cha mismu mitatu iliyopita, fall armyworm wameangamiza zaidi ya hekari 500,000 za mahindi nchini Kenya hivyo basi kuchangia kwa kiwango kikuu uhaba wa mavuno, hali ambayo imepata wakulima wakivuna pato ndogo sokoni na serikali kushinikizwa kuagiza mahindi kutoka nje ya nchi.

Ni katika hali hiyo ambapo madalali wameteka nyara sekta hiyo na kuwapuja wakulima nafasi ya kuuza mahindi yao kwa serikali, huku madalali hao wakiungana na wanasiasa kuagiza mahindi kutoka mataifa jirani na kisha kuyauzia mabohari ya serikali.

Kwa mujibu wa afisa wa ukadirjiaji ubora wa utafiti wa kiteknolojia katika Karlo, John Karanja, kwa sasa watafiti wanazingatia kuelewa jinsi dudu hili huvamia mahindi.

“Tunataka kujua kama dudu hili huja kutoka kwa mbegu za mahindi sokoni au huchipuka tu shambani katika maeneo athirika,” akasema Bw Karanja.

Alisema kuna uwezekano mkuu kuwa fall armyworm imezalishwa Kisayansi na matapeli katika soko la dawa ya kupambana na wadudu ili kujiundia soko.

“Lakini hilo ni la baadaye kwa kuwa kwa sasa kile tunajua ni kwamba dudu hili liko nasi katika sekta hii na linatesa kwa kiwango kikuu,” akasema.

Alisema kuwa washirika katika utafiti wa jinsi ya kupambana na fall armyworm tayari wamepokezwa kitita cha Sh812 milioni ili kufumbua jinsi ya kuliangamiza.

“Tuko na lengo la kuandaa mbegu ambayo katika uhai wake kutakuwa na chembechembe za sumu za kuangamiza uvamizi wa fall armyworm. Hii ni Sayansi ya mimea ambapo kuna uhandisi wa Kilimo ndani yake kuhusu mimea yaani, Seed Engineering,” akasema.

Aliambia Swahili Hub kuwa ufumbuzi huo ukiafikiwa utaambatana na ufanisi wa sasa ambapo tayari Karlo imeandaa sokoni aina nane za mbegu za mahindi zenye uwezo wa kustahimili uvamizi wa ugonjwa wa Maize lethal necrosis.

“Aina hizo nane ziko na uwezo wa kujiepusha na uvamizi wa ugonjwa huu na ziko katika usajali wa kimaeneo ambapo katika Mikoa yote minane ya hapa nchini, mbegu hizi zinaweza zikanawili,” akasema.